19 February 2013

Mbunge CCM aipa masharti serikaliNa Benedict Kaguo

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, mkoani Simiyu, Bw. Luhaga Mpina (CCM), amesema kama Serikali itashindwa kuandaa bajeti ambayo itaweza kujibu matatizo yanayolikabili Taifa kwa sasa, ataendelea
na msimamo wa kuikataa bajeti hiyo bungeni.


Bw. Mpina ni mbunge pekee wa CCM ambaye aliikataa bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13, bungeni mjini Dodoma akidai fedha zilizotengwa, hazitoshi kutekeleza mpango wa maendeleo.

Alisema hali hiyo inachangia wananchi kuichukia Serikali yao kutokana na Wizara, idara na halmashauri kushindwa kutekeleza
miradi mbalimbali ili kutatua kero walizonazo muda mrefu.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa jimbo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Mwabusalu, mwishoni mwa wiki, Bw. Mpina alisema msimamo wake wa kuikataa bajeti hiyo, hautabadilika katika Bunge lijalo la bajeti.

“Uamuzi wangu haujalenga kukihujumu chama changu bali nataka kuwasilisha kilio cha Watanzania masikini ambao wanaendelea kuishi maisha magumu kutokana na mipango mibovu ya Serikali
na fedha kidogo zinazotengwa katika mipango ya maendeleo
kushindwa kuleta ahueni ya maisha,” alisema.

Alimweleza Mwenyekiti wa CCM wilayani Meatu, Bw. Juma Mwibuli kuwa, kama mwaka huu wa fedha Serikali itawasilisha bajeti ambayo haikidhi matakwa na mahitaji ya wananchi wa
jimbo lake na nchi kwa ujumla, hataiunga mkono.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka bajeti inayoweza kujibu matatizo ya ukosefu wa ajira, bei ya mazao kama pamba na
korosho...kama itakuwa na sura hii nitaiunga mkono vinginevyo nitaendelea na msimamo wangu,” alisema Bw. Mpina.

Akizungumzia upotevu wa mapato Serikali, Bw. Mpina alisema, Kamati Maalumu iliyoundwa na Spika wa Bunge ambayo yeye alikuwa mjumbe, walibaini upotevu wa sh. trilioni nne kila
mwaka ambazo zingeweza kutumika kwa shughuli za
maendeleo ya wananchi.

Aliongeza kuwa, kamati hiyo ilibaini upotevu wa fedha hizo
ambazo hazikuwa zikikusanywa kila mwaka na kama zingekuwa zinakusanywa, zingeweza kuondoa utegemezi wa wahisani ili kusaidia miradi ya maendeleo nchini.

“Fedha hizi zingetosha kwa miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa bila wasiwasi, mazao yangepata bei nzuri na deni la Taifa ambalo kwa sasa limekuwa mzigo kwa Taifa lingepungua,” alisema.

Aliwatoa wasiwasi wananchi jimboni humo kwa kutoonekana
miezi miwili kwa sababu ya kuwa kwenye kamati ya kuangalia
jinsi Serikali inavyokusanya mapato yake na kuishauri ili
kuboresha na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumzia tatizo la uhaba wa chakula jimboni humo na
Wilaya ya Meatu, Bw. Mpina aliwatoa hofu wananchi na kudai tayari amezungumza na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda
hivyo Serikali imeahidi kupeleka tani 6,000 za chakula
cha msaada ili kupunguza tatizo hilo.

“Msihuzinike hata kama mlikosa chakula katika mgawo wa kwanza kwani Serikali ya CCM haijawasahau na chakula kitafika mapema, tatizo hili ni kubwa kwa sasa hivyo nawaomba msiuze chakula hiki.

“Kufanya hivyo, mtasababisha familia zetu zipate mateso na kushindwa kuendeleza kilimo...ila msikate tamaa ya kulima
japo mvua tunazopata za kusuasua,” alisema.

Akielezea mafanikio yaliyopo katika kata hiyo,  Bw. Mpina alisema tayari imefanikiwa kukamilisha miundombinu ya elimu kama ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Mwabusalu na ujenzi wa Kituo cha Afya Mwabusalu, ambapo ofisi yake na wadau wa maendeleo, wamechangia zaidi ya sh. milioni 50.

No comments:

Post a Comment