19 February 2013

Aliyemlisha mtoto kinyesi jela maisha



Na Esther Macha, Mbeya

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbeya, imemuhukumu kifungo cha maisha Bi. Wilvina Mkandara, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumtesa mtoto wa dada yake kwa kumlisha kinyesi, kumsababishia ulemavu wa mkono baada ya kumtia hatiani.


Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bw. Gilbert Ndeuruo ambaye alisema kuwa, mahakama hiyo imejiridhisha kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo.

Alisema mbali ya kumlisha kinyesi mtoto Aneth Johannes (3), pia alimchoma moto mkono wa kulia ambao ulioza na hatimaye kukatwa hivyo kumsababishia ulemavu wa maisha.

Hakimu Ndeuluo alisema, kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, umeithibitishia mahakama bila ya kuacha
shaka kuwa mshtakiwa alitenda unyama huo hivyo anastahili adhabu.

Alidai ushahidi uliotolewa na mashahidi upande wa Serikali, mshtakiwa hakuwa na hoja za msingi katika utetezi wake licha
ya kupinga na kudai hakumtesa mtoto huyo.

“Mshtakiwa ametiwa hatiani na kuadhibiwa chini ya sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16, kifungu cha 222(a) kama
ilivyorejewa mwaka 2002,” alisema.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Achiles Mulisa, aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho
kwa wengine wenye tabia za kunyanyasa watoto bila huruma.

Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba mahakama hiyo isimpe adhabu kali kwani alikuwa hajui mwanaye
yuko wapi pamoja na kuwakumbuka wazazi wake.

Pia mshtakiwa aliiomba mahakama hiyo imuhurumie kwa sababu alikuwa na uja uzito hivyo anahitaji muda wa kuilea mimba yake.

No comments:

Post a Comment