11 February 2013

Majibu ya Jaji Mkuu yalitikisa Bunge



Mariam Mziwanda na Grace Ndossa

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, jana alilazimika kuingilia
kati malumbano yaliyojitokeza bungeni mjini Dodoma kati ya
wabunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema.


Malumbano hayo yalijitokeza wakati Bunge likipitisha sheria mbalimbali zinazotumika kwenye mahakama nchini ambapo
baadhi ya wabunge, walidai zinawabana Waislamu katika
kesi zinazohusu imani na taratibu za dini yao.

Katika majibu yake, Jaji Werema alisema mahakama zimewapa
fursa wazee wa baraza kutoa ushauri wa maamuzi katika kesi
za kimila na zile zinazohusu dini ya Kiislamu.

Pamoja na majibu ya Jaji Weremba juu ya hoja za wabunge, Bw. Pinda alisimama na kuwataka wabunge kuelewa umuhimu wa
kazi zinazofanywa na mahakama.

Alisema wazee hao wana historia za kimila na dini hiyo ambapo
kwa mujibu wa Katiba, Serikali haina dini ila watu wake wana
imani hivyo hakuna sababu ya kuvutana.

“Hawa wazee wa baraza wamekuwepo muda mrefu...wana historia
ya mila na dini husika, unapozungumzia sheria za dini ya Kiislamu ni mambo mapana zaidi hivyo jumuku walilonalo ni kumsaidia Jaji kutenda haki kwa mlalamikaji au mlalamikiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Werema alisema mahakama ina
umuhimu wa kuwahusisha wazee wa baraza katika kesi
zinazohusu imani za dini hiyo kutokana na maamuzi yao
kukidhi mahitaji kwa kusaidia utoaji maamuzi.

Pia Bw. Werema alimtaka Mbunge wa Singida Mashariki Bw. Tundu Lissu kuwasilisha vielelezo vya mikataba ya Majaji walioajiriwa kwa mkataba ili kuthibitisha madai yake.

“Hakuna Majaji wa mikataba nchini...namuomba Mheshimiwa
Lissu alete vielelezo vinavyoonesha mikataba husika kuthibitisha
kauli yake kwani imeibuka tabia kwa baadhi ya wabunge kutumia
vipaza sauti vya Bunge kuleta siasa ili kuidharirisha mahakama.

“Kuna wakati nilitaka kurudisha cheti changu cha Sheria Chuo
kikuu cha Dar es Salaam, kwa sababu nilibaini walimu wa chuo
hiki wanahusika kuondoa maadili ya wanasheria ambao heshima
yao ni chuo alichotoa lakini walinifuata tukalimaliza,” alisema.

Jaji Weremba alisema mahakama hazipo kwa ajili ya kumtetea mtu bali zinatekeleza sheria na kuonya tabia ya wabunge kuzungumza kwa kumnyooshea kidole Spika wa Bunge kwani jambo hilo ni
utovu wa nidhamu na kumkashifu kiongozi huyo ni kukosa
uadilifu na misingi ya heshima za chombo hicho.

No comments:

Post a Comment