11 February 2013
CEGODETA yalaani vitendo vinavyotokea bungeni
Na Jesca Kileo
TAASISI ya Utawala Bora na Maendeleo(CEGODETA) imelaani na kusikitishwa na vitendo vilivyotokea hivi karibuni bungeni vilivyofanywa na baadhi ya wabunge kwenye mkutano wa Bunge uliokuwa ikiendelea Dodoma hadi kusababisha baadhi ya vikao kuairishwa kabla ya muda uliopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Bw.Thomas Ngawaiya alisema tabia iliyoanza bungeni kwa baadhi ya Wabunge kukashifiana na kufanya fujo wakati vikao vya bunge ni kinyume kabisa na misingi ya Utawala Bora,Demockasia maendeleo na inabidi Watanzania wote kukemea vitendo hivyo vya aibu bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Pia mambo wanayotenda baadhi ya wabunge bungeni sio walichotumwa na wananchi kwa maana hiyo Watanzania hawatasikitika endapo Rais ataamua lolote kwenye bunge hilo.
Bw.Ngawaiya alisema hali hiyo inaleta mfano mbaya kwa wananchi hasa kwa watoto ,vijana na wanafunzi ambao wanategemea kuwa bunge ni kioo cha jamii na ni mfano wa kuigwa kwa uadilifu,heshima na nidhamu.
"Ikiwa wanafanya vituko kama hivyo bungeni tena bunge likiwa linaendelea jamii ambayo inawatazama wao wataiga nini kwa hali hiyo ya Bunge,"alihoji na kuendelea kusema kuwa
"Nchi yetu inaheshimika dunia kote kutokana na ustaarabu wetu tulionao tangu tupate uhuru,lakini sasa kuna kila dalili ya kutoweka kwa heshima hiyo kutokana na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya waheshimiwa wawapo bungeni,"alisema Ngawaiya.
Alisema anashangaa kuona baadhi ya wabunge badala kushindana kwa nguvu za hoja wanaamua kukashifiana ,kuzomeana na kufanya fujo,mambo ambayo ni kinyume na sheria za nchi na kanuni za bunge.
Bw.Ngawaiya alisema CEGODETA inaona kuwa vurugu hizo zinazotokea Bungeni kila wakati wa Bunge zinasababishwa na baadhi ya Wabunge kutozingatia kanuni,maadili ya nidhamu ya Bunge.
Alisema CEGODETA inashangaa kwamba hakuna hatua madhubuti za kinidhamu na ikiwezekana za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wabunge husika.
Pia CEGODETA inashauri kanuni za bunge ziangaliwe upya ili kuwezesha kutoa adhabu kali kwa wabunge wanaovunja kanuni,nidhamu na maadili ya Bunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment