11 February 2013
Mnyika afichua siri miradi ya maji nchini
Na Elizabeth Joseph, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, Bw. John Mnyika, amesema miradi mingi ya maji nchini imegubikwa na ufisadi ndio maana kiti cha Spika, kimefanya juhudi kubwa za kuzima hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni ili kuinusuru Serikali.
Bw. Mnyika aliyasema hayo juzi mjini Dodoma katika mkutano mkubwa wa hadhara ulioandaliwa na uongozi wa CHADEMA
mkoani humo na kudai kuwa, agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Rehema Nchimbi kutaka vyama vya siasa visifanye mikutano ya hadhara wakati wa vikao vya Bunge, halina mashiko.
Katika mkutano huo, Bw. Mnyika alilalamikia uamuzi wa kiti cha Spika kuiondoa hoja yake aliyotaka Bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji
safi na ushughulikiaji maji taka jijini Dar es Salaam.
“Jitihada zilifanyika kuhakikisha hoja hii inazimwa kwa sababu ingeiumbua Serikali kutokana na ufisadi uliokithiri katika miradi
mingi ya maji nchini,” alisema Bw. Mnyika.
Alisema kutokana na kitendo hicho, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, amewaagiza wabunge wote wa chama hicho kuzunguka nchi nzima na kutoa ufafanuzi wa hoja husika ili
wananchi waweze kuihukumu Serikali iliyopo madarakani.
Aliwataka Watanzania hususan waishio Kanda ya Kati, kuzinduka usingizini ili kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kudai chama hicho kimeshindwa kuongoza nchi.
Aliongeza kuwa, hivi sasa nchi inatafunwa na watu wachache waliopo serikalini kwa kutanguliza masilahi binafsi na kuliacha
Taifa likiangamia bila kuchukuliwa hatua.
“Ili kuondokana na ufisadi, dhuruma na maonevu ni vyema Watanzania wakabadilika kwa kutoichagua CCM ili nchi
yetu iweze kuongozwa na chama makini.
“Hiyo yangu iliyoondolewa bungeni ilikuwa ya siku nyingi na ilipitia vigezo vyote...jambo la kushangaza inadaiwa hoja husika haikufuata vigezo vinavyotakiwa,” alisema Bw. Mnyika.
Bw. Mnyika alisema, Dkt. Nchimbi hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya kisiasa wakati vikao vya Bunge vikiendelea mjini
Dodoma kwa kivuli cha Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa mkoani humo.
“Sheria ya Usajiri wa Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992, pamoja na marekebisho yake, Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kuzuia mkutano wa siasa,” alisema.
Katibu wa CHADEMA mkoani humo, Bw. Steven Masawe, alisema sheria hiyo na ile ya Jeshi la Polisi, anayeruhusiwa kuzuia mkutano ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), ambaye anapaswa kueleza
sababu muhimu za kuzuia mkutano husika.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na ujio wa Rais katika Mkoa
au uwanja ulioombwa kwa ajili ya kufanyia mkutano huo kutumiwa na watu wengine, kama kuna mgogoro kati ya chama na chama au sababu nyingine zitakazotolewa ma Jeshi la Polisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment