20 February 2013

Majambazi wapora mil. 4/- Kibaha


Na Masau Bwire, Kibaha

WATU wanaodaiwa kuwa majambazi, wamevunja Ofisi ya
Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO), mjini Kibaha,
mkoani Pwani na kuiba sanduku lililokuwa na fedha sh. milioni 4.

Tukio hilo limetokea juzi saa 8 usiku, ambapo watu hao wakiwa
na mapanga, marungu na nondo, waliwateka walinzi wawili na kuwanyang'anya bunduki aina ya Shotgun na risasi tano.

Walinzi hao waliweka risasi hizo katika kifuko ya suruali ambapo majambazi hao waliwafunga miguu na mikono kwa kamba ya
katani na kuwaziba midomo kwa plasta.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Ulrich Matei, aliwataja walinzi hao kuwa ni Bw. Abani Sanga (66) aliyekuwa na silaha na Bw. Yusuph Kitumbo (59) aliyejeruhiwa kwa kupigwa nondo kichwani na amelazwa Hospitali ya Tumbi.

Alisema watu hao zaidi ya 15, walikata waya wa uzio katika ofisi hiyo, kuingia ndani na kufanikiwa kuwateka na kuwanyang'anya ambao inadaiwa walikuwa wamesinzia.

Aliongeza kuwa, baada ya walinzi hao kudhibitiwa, watu hao walivunja mlango wa nyuma katika ofisi hiyo, kuingia kwenye
chumba cha mauzo na kukuta sanduku la fedha lenye uzito wa
kilo 100 ambalo walilipakia kwenye gari walilokwenda nalo
na kutokomea kusikojulikana.


“Ndani ya sanduku hilo, kulikuwa na sh. 4,461,500 ambazo sh. 2,945,000 zilikuwa za matumizi ya ofisi, sh. 1,516,500 mauzo
ya maji kwa siku ya Jumamosi na Jumapili iliyopita.

“Pia watu hawa waliiba mashine mbili za mauzo (cellcom), wazitelekeza nondo walizozitumia katika uvunjaji, mkasi ambao ulitumika kukata nyaya na bunduki ya walinzi waliyoipora,” alisema Kamanda Matei.

Aliongeza kuwa, jeshi hilo linamshikilia Bw. Sanga wakati mwenzake Bw. Kitumbo, aliyelazwa Hospitali ya Tumbi baada
ya kujeruhiwa na majambazi hao akiwa chini ya ulinzi ili akipata nafuu aweze kuhojiwa kuhusu tukio hilo.

Kamanda Matei alisema, jeshi hilo linawatilia shaka watu watatu ambao walikuwa walinzi katika ofisi hiyo ambao hivi karibuni waliamua kuacha kazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kucheleweshewa malipo yao.

Hata hivyo, aliilaumu Kampuni ya Ulinzi ya S & M, yenye mkataba wa ulinzi katika ofisi hiyo kwa  kuajiri walinzi wazee ambao alisema wamechoka, hawana tena maarifa, nguvu ya kufanya kazi hiyo na kuwataka waajiri vijana wenye nguvu.

No comments:

Post a Comment