18 February 2013

Magareza yateketeza silaha haramu 3100

Peter Mwenda na Rehema Maigala

MAKAMU wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal, amesema matukio ya uhalifu wa kutumia silaha, ujambazi na uvamizi, yamekuwa yakichangiwa na wananchi wasio waadilifu, ongezeko la wamiliki wa silaha haramu.


Dkt. Bilal aliyasema hayo Dar es SAlaam jana wakati wa kuteketeza silaha haramu katika viwanja vya Kikosi Maalumu cha Jeshi la Magereza.

Alisema Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeongeza uwezo wa nchi husika kuthibiti matumizi ya silaha, kuweka kumbukumbu ya zile zinazomilikiwa na nchi husika na zilizopo mikononi mwa wananchi ili kuondoa uhalifu.

Alisema ndani ya jumuiya hiyo, kumekuwa na migogoro mbalimbali pamoja na matukio ya uhalifu ambayo mengi huchangiwa na uwepo wa silaha haramu zitapato 500,000 katika ukanda huo.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo inaonesha ipo kazi kubwa ya kukabiliana na migogoro ya uhalifu katika jumuiya hiyo.

Dkt. Bilal alisema athari ya wazi inayotokana na ongezeko la silaha haramu ni katika sekta ya utalii ambako kumekuwa na ongezeko la ujangili na uvamizi unaofanywa na mahangili katika mbuga za wanyama.

Alisema aliwakumbusha kuwa wananchi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa ulinzi wa nchi ni wa kila mmoja na wanatakiwa kuungana kukabiliana na ongezeko la silaha haramu na kutowaonea huruma wanaopjihusisha na matukio hayo.

Aliongeza kuwa, kazi ya kutunza amani inahitaji ushirikiano wa bega kwa bega na ongezeko la silaha haramu ni dosari kwa usalama wa wananchi hivyo aliwataka kuungana kudhibiti umiliki silaha usiofuata taratibu.

Aliupongeza uongozi wa jumuiya hiyo kuteketeza silaha hizo ambapo Dkt. Bilal alivuta kamba iliyofyatua bomu lililolipua bunduki na bastola za aina mbalimbali zikiwemo za kijadi 3,100.

Awali Dkt. Bilal alizikagua silaha hizo akiwa na viongozi wa jumuiya hiyo pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriiano wa Kimataifa Bw. Bernard Membe.

Balozi wa Ujerumani nchini, Bw. Klaus Peter Brandes alisema nchi yake itashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana na silaha haramu.

Alisema Serikali ya Ujerumani itaendelea kusaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki kuleta amani na ushirikiano kati ya nchi hizo za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

No comments:

Post a Comment