11 February 2013

Kuficha fedha nje si salama


Na Danny Matiko

ITAKUMBUKWA kwamba Agosti mwaka jana 2012, Waziri Kivuli wa Fedha katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zuberi Zitto, alitoa tuhuma nzito akidai kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao wameficha fedha zao nyingi kwenye baadhi ya mabenki ya nchi za nje, hususan nchini Uswissi.


Mheshimiwa Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema inakadiriwa kuwa fedha ambazo wakati huo zilikuwa zimefichwa Uswissi ni shilingi takribani bilioni 315.5.

Bw. Zitto ambaye ni Mbunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alitoa kauli hiyo wakati akichangia maoni yake kwenye hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 ambayo aliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa.

Mbunge huyo aliitaka Serikali kuchukuwa hatua dhidi ya hao aliodai wameficha fedha nje ya nchi, ikiwemo Uswissi, na kuonesha wasiwasi wake juu uhalali wa hatua hiyo.

Alisema, "iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi kuhusiana na suala hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha katika benki za Uswissi."

Miongoni mwa waliozungumzia suala hilo ni Waziri Mkuu, Bw Mizengo Pinda, aliyesema "nawaomba wabunge wenye majina ya watu hao (walioficha fedha) watuletee tuweze kuchukuwa hatua stahiki."

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw Bernard Membe, alikaririwa akisema kwamba "Serikali ipo imara na tayari kushughulikia jambo hili," akimaanisha kwamba kama Serikali ingepelekewa ushahidi wa uhakika ingeufanyia kazi na sheria kuchukuwa mkondo wake dhidi ya wahusika.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, alisema yeyote mwenye ushahidi kuhusu walalamikiwa hao aupeleke serikalini ili ufanyiwe kazi, huku Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea, akisema wao walikuwa wameiandikia barua Serikali ya Uswissi kuhusu maeneo ambayo kikosi chake kilihitaji kupata taarifa zake kwa ajili ya hatua za kisheria.

Lakini pia, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Makinda, alisema kwenye kikao hicho cha Bunge cha Agosti mwaka jana 2012 kwamba hoja hiyo ya Mheshimiwa Zitto ingepaswa kutolewa taarifa na Serikali katika kikao cha Bunge cha Aprili mwaka huu 2013 mjini Dodoma, na endapo Serikali itashindwa kufanya hivyo, basi Bunge hilo litaunda kamati ndogo ya kuzifanyia uchunguza hoja hizo.

Hivyo ndivyo ilivyoanza hoja dhidi ya hao wananchi wanaodaiwa "kuficha" mabilioni ya fedha huko ughaibuni, hususan katika nchi 11, ikiwemo Uswissi.

Sasa basi, katika hali ya namna hiyo mwelekeo unakuwa namna gani mpaka kuweza kufanikisha kurudishwa nchini fedha zilizowekwa kwenye mabenki ya nje na raia wa nchi husika?

Kwanza kabisa, katika hali ya kawaida ya kisiasa, suala hilo laweza kuonekana kama ni jepesi kwa kuwa linafurahisha kusikika masikioni kwamba watu wanabanwa ili warejeshe nchini mamilioni ya fedha walizoficha kiharamu huko nje ya nchi.

Pili, kauli hizo za kuwataka raia hao warejeshe fedha, pia linawafurahisha wanaharakati wa kisiasa kwa kuwa linachochea hamasa ya kisiasa dhidi ya upande unaolengwa na shutuma.

Lakini, katika utekelezaji wa suala hilo ndipo uhalisia wa mambo unapojitokeza na kuonesha ugumu wa aina yake.

Kama Serikali ya Tanzania yaweza kufanikisha urejeshwaji nchini fedha hizo ambazo inadaiwa ni haramu, itakuwa ni ya kwanza katika medani ya kimataifa, kwani huko nyuma serikali nyingi zilizojaribu kuchukuwa hatua ya aina hiyo ziliishia kushindwa.

Mfano hai ni serikali ya zamani ya kijeshi ya nchini Ethiopia ambayo iliongozwa na Kanali Mengistu Haile Mariam, baada ya kumuondoa madarakani Mfalme Haile Selassie mwaka 1974.

Mengistu na utawala wake waliitaka serikali ya Uswiss kurejesha Ethiopia fedha za mfalme huyo, na kudai kuwa ziliporwa (na mfalme) kutoka kwa umma wa nchi yake.

Hatimaye mamlaka ya kibenki nchini Uswissi ilijitokeza na kuitaka serikali ya Kanali Mengistu kupeleka Ulaya ushahidi usio na shaka ili kuonesha waziwazi kwamba kweli fedha hizo ziliibiwa na mfalme, na pia ushahidi huo uthibitishe na kuonesha bila shaka yoyote jinsi zilivyoporwa kutoka Ethiopia na kupelekwa Uswissi.

Hata hivyo, serikali hiyo ya Mengistu ilishindwa kuwasilisha ushahidi huo, na hivyo suala hilo kuachwa.

Kwa mujibu wa makala moja ya jarida maarufu la 'Schweizer Illustrierte' toleo la Novemba 11, 1991, lilitaja majina ya viongozi 14 wa Afrika ambao walikuwa na fedha nyingi kwenye mabenki ya nchi hiyo ya Uswissi, ambapo Mfalme Selassie alitajwa kumiliki faranga (Swiss Francs) bilioni 22.5 (wakati huu sawa na sh. trilioni 40). Kichwa cha habari cha makala hiyo kilisomeka "Laana ya fedha chafu."

Nalo shirika lisilo la kiserikali la "Global Financial Integrity" (GFI) lenye makao yake mjini Washington, Marekani, ambalo hufuatilia fedha "chafu," ikiwemo inayotokana na mikataba mibovu Barani Afrika, linadai kuwa kuanzia mwaka 1970 mpaka 2011 jumla ya dola za Marekani trilioni 5.8 (sh. zilioni 9.3 hivi) za wanansiasa wa Afrika zilifichwa kwenye mabenki ya Ulaya.

Kwa upande wa mabenki ya Uswiss, mfumo wao ni utendaji kazi kwa umoja wa kibenki, ambapo pia sekta hiyo huliingizia taifa hilo faida kubwa, ikiwemo kwa kupitia utozaji kodi na riba.

Benki yao kuu (Swiss National Bank) ilianzishwa mwaka 1906 ambapo kwa mujibu wa takwimu za kibenki za mwaka 2009 ilioneshwa kuwa sekta ya fedha nchini humo imeajiri watu 195,000, miongoni mwa hao 136,000 ni waajiriwa wa mabenki.

Kama kwamba hiyo haitoshi, mabenki ya nchi hiyo yameajiri watu 103,000 katika nchi za nje kutokana na mabenki hayo kuwa na matawi yake nje ya nchi kama ilivyokawaida kwa mabenki yote duniani.

Utafiti wa makala haya pia umebaini kuwa theluthi moja ya hifadhi ya mifuko ya fedha (world funds) kutoka jumuiya mbalimbali za kimataifa hutunzwa nchini humo, ambapo mwaka 2001 fedha hizo zilifikia dola za Marekani trilioni 2.6, huku idadi hiyo ikiongezeka  mwaka 2007 mpaka kufikia dola trilioni 6.4.

Sababu kubwa inayopelekea jumuiya na watu binafsi kutoka pande zote za dunia kupendelea kuweka fedha zao nchini Uswissi ni kutokana na imani tu kwamba kuna usalama wa fedha.

Imani hiyo imejengeka kwa miaka mingi tangu enzi ya Vita Kuu ya Pili ambapo Uswissi ilikuwa mojawapo ya nchi waathirika wakubwa kutokana na kuwa katika kitovu cha mgogoro huo.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya nchi hiyo huwa haijiingizi katika migogoro ya kimataifa, na hivyo kuonekana kama ni "eneo huria na la amani."

Hata hivyo, kuanzia mwaka 2010, sheria mpya nchini humo inatoa idhini kwa serikali, kwa kupitia mahakama, kuzuia fedha na mali zingine zitakazo lalamikiwa na nchi husika kuwa ni haramu na hivyo kutakiwa kurudishwa zilipotoka.

Miongoni mwa fedha ambazo zimekuwa za kwanza kuzuiliwa ni pamoja na za kiongozi wa zamani wa Haiti, Jean-Claude Duvalier, a.k.a "Baby Doc," na za Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbabgo, ambaye anashikiliwa na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague, Uholanzi.

Pia, fedha nyingine ambazo zimezuiliwa nchini humo kusubiri uamuzi wa mahakama ni za viongozi wa zamani, Bw Hosni Mubarak wa Misri (dola za Marekani milioni 474); Marehemu Moammer Gaddafi wa Libya (dola milioni 416 ); na Marehemu Zine el Abidine Ben Ali wa Tunisia (dola milioni 69).


No comments:

Post a Comment