19 February 2013

Kesi ya Jerry Muro yarudi tena kortini

Na Rehema Mohamed

UPANDE wa Mashitaka katika rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa Aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC) Jerry Murro aliyekuwa anakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya.


Mawakili wa wa Serikali walidai hayo jana mbele ya Jaji Fauz Twaib kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kisheria katika kuweka kumbukumbu ya Mwenendo wa
kesi hiyo jambo lililosababisha kutoa uamuzi usio wa haki.

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi alikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Novemba 30 mwaka juzi na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Frank Moshi, ambayo ilimuachilia huru Murro, Deogratius Mgasa na Edmund Kapama waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka hayo.

Katika rufaa hiyo, Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa alidai kuwa mahakama haikuandika vizuri kumbukumbu za ushahidi na vielelezo  katika Mwenendo wa kesi ambapo kuna baadhi ya
ushahidi haueleweki unamaanisha nini jambo lililosababisha Hakimu kufikia uamuzi usio wa haki.

Aidha alidai kuwa kuna baadhi ya vielelezo na ushahidi haupo kwenye mwenendo wa kesi,  ikiwemo maelezo ya onyo yaliyotolewa na Murro katika kituo cha polisi na kitabu cha wageni waliofika katika hoteli ya Sea Cliff ambayo wajibu rufaa wanadaiwa kuomba rushwa.

Aliieleza mahakama kuwa, kitabu cha wageni kilikataliwa kupokelewa mahakamani kama kielelezo lakini katika Mwenendo wa kesi haijaandikwa na hata uamuzi wa pingamizi la kielelezo hicho haukutolewa na kudai kuwa kukosekana kwa uamuzi huo kumesababisha Hakimu kutofikia uamuzi wa haki.

Aidha katika mwenendo wa kesi hakuna kumbukumbu za wao kuwasilisha Mkanda wa kamera inayonasa matukio (CCTV) ulioonesha wajibu rufaa walipokwenda kufanya
makubaliano ya kupokea rushwa, lakini walishindwa kuuangalia na  baadaye wakaamua kutumia picha za kawaida.

Aliongeza kuwa kesi hiyo awali ilikuwa inasilizwa na Hakimu Gabriel Mirunde lakini Hakimu Frank Moshi ndiye aliyetoa hukumu hivyo kutokana na kuandikwa vibaya kwa mwenendo wa kesi hiyo Hakimu Moshi alishindwa kuelewa ushahidi na utoa uamuzi usio wa haki.

Akijibu hoja wakili wa Murro, Richard Rweyongeza aliiomba mahakama kutupilia mbali hoja hiyo kwa uwa haina  misingi kisheria pia wakata rufaa hawajaeleza ni vipi kukosewa kwa mwenendo wa kesi hiyo kumesababisha kufikia uamuzi usi sahihi.

Naye Wakili wa wajibu rufaa wengine, Majura Magafu alidai kuwa wakata rufaa hawajalalamika kuhusu hukumu iliyotolewa bali maandishi katika mwenendo wa kesi  na katika hukumu hiyo hakuna sehemu ambayo Hakimu alilalamika kuwa alipata shida kusoma mwenendo wa kesi hiyo.

Alidai endapo mahakama itamua kesi hiyo isikilizwe upya itakuwa ni sawa na kufanyabiashara ya kuchagua mahakimu kuwa kama wameshindwa kwa hakimu huyo wajaribu kwa mwingine jambo ambalo haliruhusiwi kisheria.

Warufani walikuwa na sababu nne lakini imesikilizwa sababu moja ambapo baada ya kusikiliza hoja hizo Jaji Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 29 mwaka huu atakapotoa uamuzi.

Washitakiwa wanadaiwa kuwa waliomba rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage kwa lengo la kuzuia kutangazwa kwenye
televisheni habari za tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma akiwa mhasibu wa halmashauri hiyo.

Katika madai hayo, Muro na wenzake wanadaiwa Januari 28 mwaka jana jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa hilo na Januari 29 mwaka jana katika Hoteli ya
Sea Cliff Dar es Salaam waliomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa Wage.

No comments:

Post a Comment