14 January 2013

Walemavu wakiwezeshwa vitendea kazi watajikwamua kiuchumi


Na Lilian Justice

IMANI potofu kuwa mlemavu katika familia ni mkosi ni moja ya chanzo cha kuwatenga na kuwanyima huduma muhimu watu wenye mahitaji maalumu.


Baadhi ya tamaduni zimekuwa zikiwakandamiza walemavu ambapo wengi wao hufichwa ndani kwa kisingizio cha kuchekwa ama kutengwa na jamii kwa kuwa na mlemevu mmoja katika familia.

Mwamko mdogo wa jamii kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu katika jamii za kiafrika, umesababisha watu wengi kuamini kuwa mlemavu hawezi kufanya kazi yotote.

Hii inatakiwa kukomeshwa ili kunusuru kundi hilo kwani wapo walemavu ambao wanafanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko watu wenye viungo vyote.

Jamii kwa kushirikiana na serikali, taasisi binafsi inatakiwa kujenga miundombinu rafiki kwa walemavu itakayowarahisishia kupata huduma muhimu za afya na elimu ili kuondokana na adha wanayoipata pindi wanapohitaji huduma hizo.

Ingawa elimu inatolewa kuitaka jamii kutowanyanyapaa walemavu, bado kundi hilo limekuwa likibaguliwa kwa kiwango kikubwa na kukosa baadhi ya huduma muhimu na kutowapa fursa watu hao kushindwa kupata huduma hizo kutokana na miundombinu ambayo si rafiki.

Katibu wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Morogoro (CHAVITA),
Henry Mtasiwa anasema miundombinu ya majengo mengi yanayotoa huduma za afya na elimu yana ngazi badala ya lifti na kuwapa ugumu kupata huduma hizo.

Pia, katika vituo vya afya walemavu wamekuwa wakikosa kipaumbele katika suala la matibabu kwa kukosekana kwa wataalamu wa kutosha.

Anasema kuna baadhi ya  watu wamekuwa wakionesha dharau kwa jamii ya watu wenye ulemavu kiasi ambacho inawafanya kushindwa kutatua kero zao sehemu mbalimbali kama maofisini, mitaani na hata mashuleni huku baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi binafsi wakichukua fedha na
kuishia mfukoni jambo ambalo linachangia kudidimiza maendeleo yao.

Anabainisha kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa na tabia ya
kutokuwa karibu na walemavu pale wanapopewa taarifa mbalimbali zinazowahusu na kukwamisha mipango yao.

"Wakumbuke kuwa walemavu wana mahitaji yote ya kijamii kama watu wengine, serikali na taasisi binafsi zinatakiwa kuboresha na kujenga miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kupunguza changamoto zinazowakabili,"

"Walemavu ni binadamu kama walivyo wengine, hivyo tunapaswa kupewa haki zetu za msingi kama walivyo raia wengine wa nchi hii, tukumbuke walemavu hatukutaka kuwa na hali tulizonazo bali ni kwa uwezo wa muumba," anasema Mtasiwa.

Anafafanua kuwa ni vyema jamii  ifahamu kwamba ulemavu ni janga la kila mtu na kuwa si lazima azaliwe nao kwani unaweza ukawa mzima leo na kesho ukawa mlemavu kutokana na maradhi ama ajali.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kulelea watoto yatima cha Amani
Centre Padri Beatus Sewando anasema kuwa kuna baadhi ya familia akizaliwa mtoto mwenye ulemavu wanaona kama vile mkosi ama familia ina matatizo bila kujali kuwa suala la ulemavu linaweza kumfikia mtu yeyote bila kuchagua.

"Sio watu wenye ulemavu wote wamezaliwa na hali hiyo bali wapo baadhi ambao walipata wakati wakiwa na umri mkubwa, upo ulemavu wa aina tofauti, kama wa viungo, akili, ngozi, kutoongea na hata wa kutosikia.

Watu wenye ulemavu wa aina hizo zote kila mmoja anaweza kufanya shughuli zake kulingana na ulemavu wake na kwamba zipo kazi ambazo kila mmoja anamudu kufanya na kwamba isipokuwa wale wasioweza kabisa kutokana na ulemavu wao," anasema.

Mara nyingi familia za watu wenye ulemavu zinakuwa duni kutokana na walezi au wazazi kutumia muda mwingi katika kuhangaika na watoto wao kuliko kujishughulisha na kazi za kuwaingizia kipato.

Watu wenye ulemavu wa aina zote wakipata elimu kulingana na mahitaji yao wanaweza kuwa msaada kwa familia zao na kuondokana na dhana iliyozoeleka ya ombaomba hali inayowasababishia kuendelea kuwa duni katika maisha yao.

Peter Juma ambaye ni mlemavu wa viungo mkazi wa Mazimbu anasema kuwa alifanikiwa kupata elimu ya stadi za kazi katika
kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa viungo na akili cha Amani Center licha ya hali yake hiyo.

Anasema awali alikuwa hawezi kutembea kabisa na kwamba baada ya kufikishwa katika kituo hicho alipata matibabu ya viungo siku hadi siku hali yake ilizidi kuwa nafuu na hatimaye kuweza kutembea huku akipata mafunzo mengine ya stadi za kazi.

"Kama nisingepata matibabu na mafunzo yale tangu nikiwa mdogo hadi sasa ningekuwa ombaomba, lakini kwa sasa naweza kufanya kazi ndogondogo,"anasema.

Anasema alianza kazi ya kuwahudumia watu mbalimbali kwa kwenda kuwalipia bili za maji au umeme kwa ujira mdogo wa sh. 500 hadi 1000 kwa siku na kwamba fedha hiyo ilimsaidia na familia yake.

Anaeleza kuwa anategemewa na familia yake hivyo ilimlazimu kuhangaika kwa kujenga mazingira mazuri kwa jamii ili
imuamini na kumpa ujira huo aweze kupata kitu cha kumsaidia.

Kwa sasa amepata ajira ya muda katika hoteli ya Nashera kwa kufanya kazi za bustani na nyingine za nje na kupata ujira wa sh. 75,000 kwa mwezi.

Benson Nabora ambaye ni meneja katika hoteli hiyo anasema kuwa wameanzisha mpango maalumu kuwachukua watu wenye ulemavu kila baada ya miezi miwili lengo likiwa ni kutafuta watano ambao watakuwa na uwezo wa kumudu kazi za hotelini ambao watapata ajira za kudumu.

Anasema kuwa hoteli hiyo ina urafiki na mfuko wa kumbukumbu wa Erik Memorial Foundation for Education and Rehabilitation for Disabled (EMFERD) wenye kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wilayani Mvomero ambapo baada ya kutembelea waliona kuna kila sababu ya kuwasaidia katika suala la ajira.

"Kutokana na uhusiano tulionao na kituo hiki, tuliona ipo haja ya kuandaa utaratibu wa kuwapa kazi za muda na baadae tupate watano watakaopata ajira za kudumu, kazi wanazofanya zaidi ni za nje, sio kama watu wenye ulemavu hawawezi kufanya kazi wanaweza kinachotakiwa ni kuwapa nafasi," anasema.

Anaeleza kuwa watu wenye ulemavu wengi kama wakipatiwa stadi za kazi wanaweza kufanya kazi kama watu wengine.

Mbunge wa viti maalumu walemavu Magreth Nkanga anaiomba  serikali kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia kodi kampuni zinazotoa ajira kwa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwatia moyo.

Anasema hiyo itasaidia kampuni na mashirika mengine kuiga
mfano huo lengo likiwa ni kumkomboa mlemavu kutoka katika wimbi la tegemezi ambapo wengine kutengwa hata na familia zao kwa kuogopa mzigo.

Mhando Kigolo, Afisa Ustawi wa Jamii katika kituo hicho anasema kwa sasa wapo watu wenye ulemavu 150 kituoni na kwamba wamekuwa wakiwapatia stadi za kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ng'ombe na kuku, ufumaji na suala zima la ujasiriamali lengo likiwa ni kupata ajira.

"Tumekuwa tukiwashirikisha wazazi na walezi wa watoto hao ili wajue wajibu na hali za watu hao wenye ulemavu na kuweza kuwasemea kwani wao ndio wanastahili na hiyo pia inatusaidia kutupatia ushirikiano kufanikisha malengo yetu," anaeleza.

Mshauri wa kituo hicho Josephin Bakita ambaye ndio mwanzilishi wa kituo hicho anasema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2003, kutokana na mtoto wake aliyekuwa mlemavu wa viungo kufariki.

Anasema kila anayeguswa na walemavu atakuwa akiwathamini na kuwasaidia, kwani ni watu wanaohitaji huruma wakati wote na misaada kulingana na hali zao na sio watu wa kunyanyapaliwa kama baadhi wanavyowachukulia na kuonekana hawana mchango wowote.

Ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha inaweka mikakati
itakayowajengea mazingira rafiki walemavu katika sekta zote ili kuwasaidia kupata huduma stahiki pindi wanapohitaji sambamba na kutoa elimu kwa umma kuacha kuwatenga.

No comments:

Post a Comment