16 January 2013

Wakulima wapewe elimu ya kilimo cha kisasa



KILIMO kwanza ni mpango unaotekelezwa na Serikali ili kuhamasisha wakulima waongeze juhudi kwenye kilimo cha kisasa, kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini.

Lengo la mpango huo ni kuleta mapinduzi ya kijani katika sekta ya
kilimo kiuchumi na kijamii lakini tangu kuanzishwa kwake, zipo kasoro nyingi ambazo zinahitaji kutatuliwa mapema ili tusipoteza maana halisi ya mpango husika.

Baadhi ya wadau wa kilimo, wamekuwa wakionesha waiswasi wao juu ya kufanikiwa kwa mpango huo kutokana na kasoro zilizopo.

Serikali imekuwa ikipiga kelele na kuwataka wananchi wake kujikomboa kiuchumi kupitia mpango huo. Ukweli ni kwamba,
bila kutatua kasoro zilizopo mpango huo hauwezi kufanikiwa
kama unavyotarajiwa.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania bado ina safari ndefu ili kufanikisha mpango huo. Dhamira na utashi katika mkakati huo ni nzuri ili kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo na kukuza uchumi.

Tatizo kubwa linalokwamisha mpango huo ni siasa, baadhi ya viongozi wanasimama jukwaani kuufagilia wakati wao wenyewe wanafahamu wazi kuwa bila miundombinu ya barabara hasa ziendazo vijijini, mpango huo hauwezi kufanikiwa.

Barabara zilizopo hazipitiki kirahisi hivyo kusababisha pembejeo zishindwe kufita kwa wakati sambamba na wakulima kushindwa kupeleka mazao yao sokoni kutokana na ubovu wa barabara.

Baadhi ya wataalamu wa kilimo, hawana utamaduni wa kuwafikia wakulima vijijini ili kuwapa maelekezo ya kilimo cha kisasa jambo linalochangia malengo ya mpango huo kukwama.

Tatizo jingine ni ukosefu wa soko la uhakika ambapo mazao mengi huaribika shambani kabla ya kufika sokoni hivyo kusababisha harasa kubwa kwa wakulima waliotumia muda mwingi kukaa shambani.

Licha ya changamoto hizo, wakulima wengi hawana mbinu za
kisasa za uvunaji na uhifadhi mazao yao kabla ya kufikishwa
sokoni. Uchafu wa mazao na uhifadhi duni, pia husababisha wakulima wakose soko la uhakika.

Katika maeneo mengi, wakulima wamewekeza vikwazo vya kupata mikopo na taasisi za fedha ili kukuza mitaji yao, kuongeza mashamba na kununua pembejeo za kutosha.

Upo umuhimu mkubwa wa Serikali kuhakikisha wakulima wetu wanapewa elimu ya kilimo cha kisasa ili wapate mazao yenye kukubalika kwenye soko.

Serikali iweke mpango maalumu wa kuboresha barabara hasa ziendazo vijijini ambako ndiko kuna wakulima wakubwa na wadogo, kutoa elimu ya kilimo cha kisasa na kuwawezesha pembejeo za kilimo kwa gharama nafuu.

No comments:

Post a Comment