14 January 2013

Sumaye awashukia wapinzani



Na Kassim Mahege

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amewaonya wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaotumia mgogoro wa gesi mkoani Mtwara ili kutaka kujipatia umaarufu kwa wananchi.

Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na gazeti hili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, kabla ya kupandandege kwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za miaka 49 ya Mapinduzi, yaliyofanyika Januari 12,1964.

Alisema gesi inayotaka kusafirishwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni sawa na tone la maji ukilinganisha na iliyopo hivyo ni vyema Serikali ikatoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa dhamira ya kusafirisha gesi hiyo kwa faida ya Watanzania wote.

“Kinachofanywa na wanasiasa wa vyama vya upinzani ni kuwapandisha hasira wananchi wa Mtwara kwa kuwajaza
maneno ili waichukie Serikali ya chama tawala CCM.

“Hakuna sababu ya wanasiasa kutafuta umaarufu kwa kuwajaza maneno wananchi ili waichukie Serikali, jambo hili si sahihi na halipaswi kuendelezwa katika nchi yenye misingi mizuri ya
amani na utawala bora,” alisema Bw. Sumaye.

Aliongeza kuwa, kama gesi ya Mtwara itazuiwa kusafirishwa hadi Dar es Salaam, wakazi wa Mtwara hawataimaliza hivyo jambo la msingi ni kuitumia kwa manufaa ya Watanzania wote.

Alitolea mfano wa zao la ndizi linalolimwa Bukoba, mkoani Kagera na Moshi, mkoani Kilimanjaro, maharage yanayolimwa Mbeya na korosho za Mtwara vyote vinaliwa jijini Dar es Salaam, ambako
ndio kitovu cha uchumi wa Taifa.

“Kuna rasilimali nyingi sana katika nchi yetu, watu waishio jirani
na Bwawa la Mtera na Nyumba ya Mungu wakisema maji yake yasitumike kuzalisha umeme itakuwa sahihi? alihoji Bw. Sumaye.

Alisema msingi wa Taifa lolote duniani ni umoja, ushirikiano na amani ambapo jambo lolote linaloweza kuhatarisha umoja wa wananchi kwa kuhusisha rasilimali za nchi linapaswa kukemewa.

Akiuzungumzia mwaka 2012, Bw. Sumaye alisema changamoto mbalimbali zilijitokeza ikiwemo migogoro ya wafugaji, wakulima na ubaguzi wa dini hivyo aliitaka Serikali kuhakikisha mwaka 2013, inarekebisha kasoro hizo.

“Wito wangu kwa Watanzania wafuate sheria bila kushurutishwa, suala la mgombea binafsi katika Uchaguzi Mkuu ujao siwezi kulizungumzia, wakati ukifika Watanzania watamchagua
mgombea anayefaa kuwaunguza,” alisema

No comments:

Post a Comment