14 January 2013
Walimu wakimbia shule wakihofia kuuawa
Na Jovither Kaijage, Ukerewe
WALIMU watano wa Shule ya Sekondari Bwisya Kisiwani Ukara, iliyopo Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, wamekimbai shuleni hapo wakihofia kuuawa na wezi wanaovamia nyumba zao mara
kwa mara, kuiba mali pamoja na fedha.
Mkuu wa shule hiyo, Bw. John Lunguya, aliyasema hayo jana kwa waandishi wa habari mjini Nansio na kuongeza kuwa, walimu wanne wamekataa kuludi shuleni hapo baada ya kwenda likizo.
Alisema usalama wa walimu wa shule hiyo si mzuri kutokana na kasi ya matukio ya kuvamiwa katika nyumba zao hasa nyakati za usiku ambapo mwaka 2012, yalitokea matukio mawili tofauti ya kuvamiwa kwa walimu wa shule hiyo.
Aliongeza kuwa, tukio la kwanza lilitokea Aprili mwaka huu ambapo Mwalimu John Michael, alivamiwa usiku na kuibiwa
fedha za shule sh. 700,000 wakati Mwalimu Likenji Kindamba, akiibiwa sh. 85,000 alizopokea kwa wanafunzi wa bweni.
“Mimi mwenyewe nilivamiwa nyumbani kwangu ambapo wezi waliiba sh. milioni 2.8 za biashara yangu ya kuuza bia na Mwalimu Deogratius Malima, akivamiwa na kuibiwa kamera ya kisasa ambayo inapiga picha za mnato,” alisema.
Bw. Lunguya alisema, Desemba 2012 alivamiwa tena na wezi nyumbani kwake lakini hawakufanikiwa kuiba chochote hivyo ameamua kuikimbia nyumba yake na hivi sasa anishi katika
nyumba ya kulala wageni pamoja na familia yake.
“Walimu wenzangu wameamua kwenda kuishi mjini Nansio
kwa marafiki zao wakihofu kuuwa,” alisema Bw. Lunguya.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Sekondari wilayani humo, Godrive Nnko, alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kudai
kuwa, juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwashawishi walimu hao waweze shuleni hapo na kuendelea kufundisha.
“Wakazi wa eneo hili wameahidi kuimarisha ulinzi hivyo tumefurahishwa na uamuzi wao ndio maana tunajitahidi
kuwahamasisha walimu warudi kazini,” alisema.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Mery Tesha, alisema tayari amepokea taarifa hizo na kusisitiza kuwa, anakusudia kwenda kisiwani hapo
ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Mangu, alisema tayari amemtuma Mkuu wa Polisi wilaayani humo Bw. Shitambi Shilogile kwenda kiwasiwani hapo ili kuchunguza tukio hilo lakini alionesha wasiwasi wa walimu hao kutafuta kisingizio cha kutaka wahamishwe kituo cha kazi.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), wilayani humo, Bw. John Kafimbi, amelaani vikali matukio hayo, kuvilaumu vyombo vya dola pamoja na jamii jamii ya eneo hilo kwa
kushindwa kuwalinda walimu na familia zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment