03 January 2013
Kinondoni kuongeza nguvu kushughulikia kero ya ardhi
Na Goodluck Hongo
MANISPAA ya Kinondoni imewataka wananchi kutoa ushirikiano wa hali na mali katika mapambano dhidi ya migogoro ya ardhi na watu wote wanaokwenda kinyume na utaratibu wa kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam juzi na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Fortunatus Fwema alisema manispaa hiyo imeahidi kuongeza nguvu katika kushughulikia masuala ya migogoro ya ardhi katika manispaa hiyo.
Alisema katika kukabiliana na migogoro hiyo, uongozi wa manispaa umekuwa ukichukua hatua za haraka kuhakikisha viongozi na watendaji wanaojihusisha na migogoro na kashfa za ardhi wanachukuliwa hatua stahiki.
Alisema katika kuishughulikia migogoro hiyo, manispaa imekuwa ikiendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya kamati ya migogoro ya ardhi iliyoundwa kwa maelekezo ya rais, hatua aliyodai kuwa kwa kiasi kikubwa imeweza kuleta mafanikio.
"Hadi sasa migogoro iliyokuwepo imeshughulikiwa kwa asimilia 95 na kupatiwa ufumbuzi na migogoro iliyopo ni ile inayotokana na uvamizi wa ardhi unaofanywa na makundi ya watu kinyume na sheria ambayo manispaa kwa kushirikiana na Serikali kuu imeendelea kuipatia ufumbuzi," alisema Fwema.
Aidha aliwataka baadhi ya wananchi kuacha kuwa na mawazo yasiyo na msingi kuwa manispaa hiyo imekuwa ikifanya upendeleo kwa wakubwa wakati wa uuzaji wa viwanja vyake jambo ambalo halina ukweli.
"Madai haya si ya kweli ikizingatiwa kuwa katika kipindi kinachokaribia miaka 10 manispaa ya Kinondoni haijawahi kupima viwanja na kuviuza kwa wananchi kutokana na changamoto mbalimbali hasa zinazohusiana na utwaaji wa ardhi na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kugharamia fidia na upimaji, " alisema Fwema.
Alisema manispaa kwa muda mrefu imekuwa ikihangaika kutafuta fedha za kupimia viwanja kutoka sehemu mbalimbali zikiwemo taasisi za fedha na madhumuni ni kuvipima viwanja hivyo ili kukabiliana na ongezeko la ujenzi holela katika maeneo yasiyopangwa.
Kuhusu utoaji wa vibali vya ujenzi na kushughulikia maombi ya kubadili matumizi ya ardhi,Fwema alisema manispaa hiyo kwa kutumia wataalam wake, kabla ya kutoa vibali hivyo wameweka utaratibu wa kuhakikisha maombi yaliyotolewa, hayakinzani na matumizi yaliyopo na yaliyoidhinishwa katika mpango wa matumizi ya ardhi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment