03 January 2013

Viongozi Temeke washauriwa kutembelea miradi



Na David John

VIONGOZI wa Halmashauri ya Temeke wameshauriwa kujenga dhana ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya manispaa hiyo na si kujiridhisha na taarifa za kwenye vyombo vya habari.

Ushauri huo umetolea Dar es Salaam jana na diwani wa kata ya Kimbiji,Kigamboni Wilayani Temeke, Muhidin Sanya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na changamoto anazokabiliana nazo katika kata yake.

Alisema viongozi wa manispaa hiyo wamekuwa wakiridhika na taarifa za kusoma kwenye magazeti, na kusikiliza redio pasipo kuchukua hatua za kutembelea miradi hiyo ili kuona utekelezaji wake.

"Viongozi wanabweteka na taarifa za kwenye magazeti na radio mwisho na ndio maana hawana utamaduni wa kwenda kutembelea miradi hiyo na mwishowe taarifa zinabainika kutokuwa na ukweli,hivyo ninawashauri kubadilika na si kubweteka maofisini tu, " alisema.

"Ndani ya Kata ya Kimbiji ilipewa taarifa kuwa mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Bohari umekamilika vyumba viwili vya madarasa na vyumba hivyo vimegharimu sh.milioni 36 taarifa ambayo haikuwa ya kweli jambo ambalo limerudisha nyuma maendeleo,"alisema.

Alisema baada ya kugundua taarifa hiyo si ya kweli wakajaribu kufanya marekebisho ya taarifa hiyo,  na kuongeza kuwa taarifa hiyo ili kuwa imekosewa,nakudai vyumba hivyo vipo mbioni kujengwa.

Diwani Sanya alisema inasikitisha kwa sasa kuona chumba kimoja cha darasa kinatumiwa na mikondo minne hali ambayo inasababisha wanafunzi kuzurura nje ya eneo la shule na wengine kuishia mitaani.

Aliongeza kuwa shule hiyo mbali ya kuwa na chumba kimoja pia ina matundu mawili ya choo ambayo  kimsingi hayakidhi mahitaji ya wanafunzi wote shuleni hapo.

Akizungumzia changamoto hizo Ofisa elimu wa Manispaa ya Temeke Honolina Mumba alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuongeza kuwa ni kweli taarifa iliyotolewa kuhusu ujenzi wa shule hiyo ilikuwa imekosewa na kwamba shule hiyo ya Bohari inachumba kimoja na ujenzi wa vyumba vingine viwili unatarajiwa kuaza na tayari tenda ya ujenzi imeshatangazwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment