18 January 2013

Katiba Mpya iwabane na kukomesha uzembe kwa watendajiTaasisi na viongozi mbalimbali waliopo serikalini na wastaafu,
wapo katika mchakato wa kutoa maoni ya Katiba Mpya kwa
Tume anayoratibu mchakato huo jijini Dar es Salaam.


Jamii kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, inalalamikia utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji serikalini ambao kwa kiasi kikubwa wanachangia kukwamisha maendeleo ya sekta mbalimbali.

Wapo baadhi ya watendaji wanaotumia nafasi walizonazo kujinufaisha kama inavyoripotiwa katika vyombo juu ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali ambazo ni kodi za wananchi.

Katiba ni mfuko wa kanuni ambazo zinaongoza dola na kutoa mwongozo wa taratibu za mfumo wa Taifa kujitawala kwa mujibu wa kanuni na sheria ili kubaini wajibu na haki kwa watawala na watawaliwa.

Baada ya shughuli za binadamu kuongezeka ili kujikwamua na umaskini katika mazingira anayoishi, likaingia suala la ubinafsi
wa kujimilikisha njia kuu za uzalishaji mali.

Hali hiyo ilichangia ukandamizaji, unyonyaji na ufedheheshaji wanyonge ambao walinyimwa haki kwa misingi ya kibaguzi.

Tatizo hilo lilichangia uzalishaji mali kuwa wa kitabaka, ongezeko la migogoro ya haki, usawa na kugawana ziada iliyopatikana katika uzalishaji.

Migogoro hiyo ilifanikiwa kuangusha mifumo kandamizi lakini bado uhusiano wa kitabaka uliendelea kuwepo. Jamii kubwa imekosa haki ya kutumia rasilimali za nchi kwa tamaa na ubinafsi. Hiki ndicho kitatokea kwa kizazi cha sasa ambacho kinadai Katiba Mpya.

Angalizo ni kwamba, kama katiba haitakidhi matakwa ya wananchi, watakuwa na uamuzi wa woga hivyo kufungua kitanzi cha umaskini, ujinga na maradhi.

Katiba Mpya inapaswa kulinda rasilimali za Taifa kwa masilahi ya Watanzania wote na kuzingatia maoni ya wananchi ili kuchochea maendeleo ya jamii na sekta mbalimbali.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania ina rasilimali nyingi za kuweza kuhudumia wananchi wake. Taifa lenye vipaumbele vya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na teknolojia, mafanikio yake yatatokana na sheria imara ambayo ni katiba.

Katiba Mpya iwawajibishe watendaji wa Serikali na wananchi wanaotumia rasilimali za nchi kujinufaisha na izingatie demokrasia kwa watu wenye mapenzi mema kwa faida ya Taifa lao.

Tungependa kuona Katiba Mpya inakomesha uzembe katika utendaji kazi wa shughuli za maendeleo kwani Tanzania ni nchi yenye neema lakini wananchi wananung'unika kutokana na ugumu wa maisha.

Imani yetu ni kwamba, wananchi wana nguvu ya kuzalisha mali ila bado wanateseka kwa sababu ya kukosa katiba yenye usawa na haki.

No comments:

Post a Comment