18 January 2013
JK amtembelea DCI Manumba, bado kalazwa ICU
Na Goodluck Hongo
RAIS Jakaya Kikwete, jana alikwenda kumjulia hali Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi nchini, DCI Robert Manumba, ambaye amelazwa katika chumba cha watu mahututi (ICU), kwenye Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam.
Katika hospitali hiyo, kulikuwa na maofisa mbalimbali wa jeshi hilo ambapo Rais Kikwete aliwasili hospitalini hapo saa jioni akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete.
Baada ya kuwasili, waliingia moja kwa moja ICU ili kumuangalia mgonjwa na kupata maelezo ya madaktari wanaomuhudumia.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tiba hospitalini hapo, Dkt. Jaffer Dharsee, alisema DCI Manumba bado ameendelea kulazwa katika hospitali hiyo akipatiwa matibabu.
“Hali yake kiafya bado inahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi,” alisema Dkt. Dharsee ambaye katika taarifa yake, haikuonesha ugonjwa unaomsumbua DCI Manumba.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, akiwa na maofisa wengine wa jeshi hilo, naye alifika hospitalini hapo ili kumjulia hali DCI Manumba na baada ya kutoka, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, taarifa zote watazipata kwa uongozi wa hospitalini hiyo.
“Waandishi tumekubaliana kuwa taarifa zote zitatolewa na uongozi wa hospitali kuhusu hali ya mgonjwa lakini mkae tayari kwani Rais atakuja, alipata dharula kidogo lakini,” alisema IGP Mwema.
Bw. James Kiraba ambaye ni msemaji wa familia ya DCI Manumba, alisema hali yake inaendelea kuimarika hivyo jambo la muhimu ni kuzidi kumuombea ili aweze kupona kabisa.
Msemaji wa jeshi hilo, Bi. Advera Senso hakuweza kuzungumza chochote juu ya hali ya DCI Manumba ambapo baadhi ya maofisa wa polisi waliokuwepo hospitalini hapo ni pamoja na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment