18 January 2013

Mchina jela miaka 3 akimpa rushwa DC



Na Raphael Okello, Bunda

MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, imemuhukumu raia wa China, Bw. Mark Wang Wei (30), kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. 700,000, baada ya kutiwa hatiani na kosa la kutaka kutoa rushwa ya sh.500,000 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Bw. Joshua Mirumbe.


Bw. Wei alifikishwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), wilayani humo ambapo Mwanasheria wa taasisi hiyo, Bw. Mwema Mella,
alisema Bw. Wei, alitenda kosa hilo Januari 16 mwaka huu,
saa 7:30 mchana, akiwa katika ofisi ya Bw. Mirumbe.

Bw. Mella alisema Bw. Wei ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Panda International Company LTD ya mjini Shinyanga, inayohusika na uzalishaji pamoja na usambazaji wa pembejeo za kilimo.

Alidai kuwa, Bw. Wei alitaka kutoa rushwa kwa Bw. Mirumbe
kwa ajili ya ushawishi wa kampuni yake iweze kupata zabuni
ya usambazaji wa pembejeo wilayani humo.

Aliongeza kuwa, baada ya Bw. Mirumbe kubaini uwepo wa mazingira ya rushwa, alitoa taarifa kwa Maofisa wa TAKUKURU ambao waliofika ofisini kwake na kuweka mtego uliofanikiwa kumnasa Bw. Wei.

Akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Safina Semfukwe, mshtakiwa ambaye alikuwa akizungumza Kingereza
kwa tabu kutokana na Mahakama hiyo kukosa Mkalimani wa lugha ya Kichina, alidai hakujua kama kufanya hivyo kwa mtu rafiki ni kosa.

Alidai nchini kwao China, kufanya hivyo ni kitendo cha kawaida kwa mtu aliye rafiki hivyo aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu ombi ambalo liliungwa mkono na Mwanasheria wa TAKUKURU ambaye alisema, Bw. Wei hakuwasumbua
wakati wakimuhoji.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Semfukwe aliyeonekana kuguswa na ombi la Bw. Wei, alisema kitendo cha mshtakiwa kutokujua sheria hakimwondoi kwenye hatia na kutoa hukumu hiyo.

Hata hivyo, Bw. Wei alilipa faini hiyo ya sh. 700,000 na kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela.

Juzi Bw. Mirumbe alikataa kupokea rushwa ya sh. 500,000, kutoka kwa Bw. Wei ili kampuni yake iruhusiwe kusambaza pembejeo kwa wakulima wilayani humo na kudai fedha hizo alizitoa kama zawadi.

Alisema kampuni yake iliwekwa kwenye orodha ya kuomba zabuni ya kusambaza pembejeo za kilimo mkoani humo na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Aliongeza kuwa, Bw. Wei alimwandikia ujumbe mfupi wa maneno (sms), katika simu yake ya mkononi akitoa ahadi ya kwenda kumpa zawadi.

“Jambo hili lilinipa shaka kwani sikuwa na ahadi yoyote kutoka kampuni hii hivyo nilitoa taarifa TAKUKURU ambao waliweka mtego ofisini kwangu na kumkamata Bw. Wei.

Alisema kabla Bw. Wei hajakamatwa, alikwenda ofisini kwake kupeleka barua kutoka Uhamiaji ikimtambulisha kuwa yeye ana kibali cha kuishi nchini hadi Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua kutoka Uhamiaji, Bw. Wei aliandikiwa kibali kutoka mkoani Shinyanga chenye pasi namba 000004729, ambacho kinamruhusu kukaa na kufanyakazi nchini hadi Machi 15,2013.

Awali Bw. Wei alikuwa na kibali kilichokua kinaishia Januari 15 mwaka huu hivyo wakati alipofika kwenye kikao cha pamoja,
kibali chake kilikuwa kiishe baada ya siku 10.

“Kwa sababu muda wa kuisha kibali chake ulikuwa umekaribia, tulishindwa kumpa zabuni ya kusambaza pembejeo wilayani hapa kabla ya kuleta kibali kipya na sh. 500,000,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Kilimo wilayani humo, Bw. Masuke Ogwa, kampuni hiyo ilikuwa haijaruhusiwa kusambaza pembejeo wilayani humo kutokana na sababu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment