14 January 2013

Israel wafurahia msimamo wa Tanzania


Na Danny Matiko

WANANCHI nchini Israeli wamefurahia msimamo wa serikali ya Tanzania dhidi ya usajili wa meli za Iran nchini, ambapo pia inaelezwa kuwa usajili huo sasa umefutwa.


Furahi hiyo ya Waisraeli inatokana na kinachoaminika kuwa ni juhudi za kimataifa dhidi ya tishio la mara kadhaa kutoka serikali ya Iran kwamba yaweza kutumia silaha za maangamizi, ikiwemo nyukilia, kuiteketeza nchi hiyo ndogo na hivyo kuifuta kutoka Ramani ya Dunia.

Madai hayo ya Iran na yale ya nchi hiyo kudaiwa kumiliki silaha hatari za maangamizi, ambayo inayakanusha, Umoja wa Mataifa (UN) uliamua kuiwekea vikwazo vya kiuchumi kwa lengo kuidhoofisha.

Azimio la vikwazo hivyo ni namba 1929 la mwaka 2010 la ambalo lilipitishwa kwa kura za wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), mjini New York, Marekani, Juni 9, 2010.

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama ambazo zilipiga kura zilikuwa 15, ambapo 12 zilikubali, mbili (Brazili na Uturuki) zilipinga, na moja ambayo ni Lebanon ilikwepa kupiga kura.

Brazili ilidai kuwa ni vyema Iran iachwe ijenge vinu vya nyuklia ili kushughulika na urutubishaji wa madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya nishati ya umeme.

Ilidai kuwa matumizi hayo si ya kimaangamizi, na kwamba "kurutubisha urani si kigezo kwamba nchi inamiliki silaha za nyuklia."

Nchi ambazo zilipitisha azimio hilo ni pamoja na zile za kudumu kwenye Baraza hilo ambazo ni China, Marekani, Ufaransa, Urusi, na Uingereza.

Nyingine ni zile ambazo ilikuwa ni zamu yao kuwemo kwenye Baraza, nazo ni Australia, Japan, Mexico, Bosnia, Gabon, Nigeria, na Uganda.

Kadhalika, ni katika Azimio hilo ndimo inatajwa kuwa Irani izuiwe kusafirisha mafuta yake kwenda soko la kimataifa, ambapo pia, pamoja na vikwazo kibao, Azimio linazitaka "serikali zote kusaidiana kuibana kiuchumi nchi hiyo ambayo ni namba moja kwa uzalishaji wa mafuta duniani.

Wafuatiliaji wa mambo hushindwa kuelewa sababu iliyosababisha nchi rafiki wa Iran kwenye Baraza la Usalama, ambazo ni China na Urusi, kushindwa kukataa nchi rafiki yao kuwekewa vikwazo hivyo.

Ni kwamba "zilishindwa kisiasa" kwa sababu Marekani ilieleza kwenye baraza hilo kwamba "Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia ili hatimaye iweze kuzitumia kuiteketeza Israeli, na pia, kama ikibidi, kuweza kuipiga nchi yoyote itakayohitilafiana nayo duniani.

Mataifa ya Magharibi, yakiongozwa na Marekani, yakawaeleza wajumbe wa UN kwamba endapo Baraza la Usalama lisingechukuwa hatua dhidi ya programu hiyo ya kuunda silaha za kuangamiza halaiki, hatimaye tishio la Iran lingekuwa ni kwa dunia nzima.

Hivyo basi, Urusi ambayo inapakana na Iran, kimsingi iliona hatari hiyo,  na kadhalika China ambayo mji mkuu wake, Beijing, upo umbali wa kilometa takribani 5,600 za anga kutoka mji mkuu wa Iran, Tehran, na yenyewe ilipata hisia ya tishio hilo.

Tukumbuke kuwa mwendo kasi wa kawaida wa ndege kutoka Tehran mpaka Beijing ni takribani saa 7, ambapo bila shaka yoyote ndege yenye kombora la nyuklia yaweza kusafiri kwenda huko na kurusha kombora hilo na kutoroka kurudi ilikotoka.

Tishio ni kwamba kama leo nchi moja na nyingine ni marafiki, lakini hali hiyo ya amani yaweza kuvurugika na kuwa tata endapo utazuka utawala mpya wenye sera tofauti katika nchi hizo; ambapo kama kuna moja yenye nyuklia, ni kwamba tishio laweza kuwa kubwa.

Kufurahishwa kwa wananchi wa Israeli kunatokana na Tanzania ilivyoshughulikia suala la meli hizo, ambapo wamekuwa wakitoa maoni yao kwa kupitia kurasa za magazeti ya nchi hayo.

Gazeti kubwa la nchi hiyo, "Jerusalem Post," ambalo lilianzishwa mwaka 1932 likijulikana kwa jina la "Palestine Post", kabla ya kubadilishwa jina mwaka 1950, wiki iliyopita lilirudia kunukuu kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd, aliyoitoa mwishoni mwa mwaka jana kwenye Baraza la Wawakilishi akisema kwamba Zanzibar ilikuwa katika hatua ya kuzifutia usajili meli zote za Iran ambazo zilisajiliwa Visiwani humo isivyohalali.

Gazeti la "Haaretz", huku likikariri hotuba ya Balozi Seif, liliandika kuwa "tishio la kutaka kuangamiza nchi nyingine kwa silaha za kemikali au nyuklia linahuzunisha, lakini pia pale jamii ya kimataifa inapojitokeza kusaidia instahili kupongezwa.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine ambazo zimetangaza kuzifutia usajili meli za mizigo za Iran ni Sierra Leone, Visiwa vya Tuvalu (katika Bahari Kuu ya Pacific), Hong Kong, Cyprus, na Malta.

Nchi zote hizo zimekuwa zikidai kuwa kulikuwa na njama za udanganyifu wakati wa kusajili meli hizo.

Mwaka jana Kenya ilifuta mkataba wa uagizaji mafuta kutoka Iran, ambapo katika makubaliano ya awali, nchi hiyo ingenunua mafuta tani milioni 4 kwa mwaka.

Taarifa ya serikali ya Kenya ilisema "licha ya tukio hili, uhusiano wetu na Iran utabaki kuendelea kama kawaida katika maeneo na sekta nyingine."

Wakati hali ya mambo ikiendelea hivyo, taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa shughuli za kiuchumi za Iran zinaendelea kama kawaida, ambapo serikali ya nchi hiyo ilitangaza Jumatano, Januari 9, mwaka huu, kwamba biashara yake ya nje katika kipindi cha miezi 3 iliyopita imeingizia nchi hiyo zaidi ya dola za Marekani bilioni 73.

Taarifa ya serikali ilisema katika fedha hizo dola bilioni 42 zilihusika katika kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ofisa wa ngazi ya juu katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaji ya Kibiashara ya Iran (TPOI), Kioumars Kermanshahi, alisema, licha ya kuwepo vikwazo vya kimataifa, nchi yake bado ipo imara kiuchumi.

Hata hivyo, wakati sakata hilo la usajili wa meli za Iran likiendelea duniani, yameibuka madai mengine kwamba nchi hiyo imevuruga mfumo wa ishara za kimawasiliano kwa njia ya setelaiti kiasi kwamba ufuatiliaji wa meli zake kubwa umeingiwa na dosari.

Wachambuzi wa taasisi ya "Fairplay (IHS) ambayo inafuatilia nyendo za meli kubwa za kimataifa baharini, wanaeleza kuwa meli za Iran kwa sasa hutumia ishara za meli nyingine, ambapo hiyo huzifanya kusomeka kwenye mitambo ya setelaiti kwa majina bandia.

Mfano ni kwamba kama jina la meli ya nchi nyingine ni "KBC" na ya Iran ni "Kurks", jina la meli ya Iran halinaswi kwa njia ya setelaiti isipokuwa jina la "KBC" ndilo huonekana.

Hiyo ikiwa na maana kwamba kama meli kubwa ya Iran, "Kurks," ipo katika bahari ya Japan, uwepo wake huko hautasomwa na setelaiti isipokuwa jina litakaloonekana ni la meli "KBC," ambayo sio ya Iran.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba, setelaiti itaonesha kuwa kuna meli mbili baharini ambazo zinatumia jina moja la "KBC."

Hakika, teknolojia hiyo ya hali ya juu inatisha, na inaifanya hata Israeli kujiweka tayari kutokana na vitisho vya Iran.

Tukiachana na sura hiyo mpya katika ukwepaji wa mkono wa sheria za kimataifa, kwa upande mwingine, Januari 7, mwaka huu, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, akihutubia zaidi ya watu 3,000 mjini Jerusalemu alisema kwamba Iran na rafiki yake Syria ni tishio kubwa kwa dunia.

Akihutubia kwa lugha ya Kiingereza huku akishangiliwa kwa vifijo na nderemo, Waziri Mkuu huyo aliwaambia machotara hao wa Kiyahudi kwamba "hebu tupeane ahadi hapa kwamba tutapigania kuwepo amani, ambapo dunia ni budi iamke na kupambana dhidi ya hatari kutoka Iran na Syria."

No comments:

Post a Comment