14 January 2013
Matokeo darasa la saba tumevuna tulichopanda
Na Aziz Msuya
MATOKEO ya Darasa la Saba kwa Mwaka 2012 yametoka yale niliyoyatabiri muda mfupi kabla ya wanafunzi hao kuingia kwenye mtihani huo wa kumaliza elimu ya Msingi yametokea,wanafunzi wengi wa shule za Serikali wamefanya vibaya ukilinganisha na shule binafsi.
Sababu za wanafunzi hao kufeli ziko wazi kabisa,sababu ya kwanza ni mfumo uliotumika kufanya mitihani hiyo maarufu kama “kusiliba” au ku “shade” mfumo huu umeathiri wanafunzi wengi na hasa wa vijijini ambao hawakupata muda wa kufanya mazoezi mengi ili kuwafanya wauzoee mfumo huo mpya ingawa kwa wasahihishaji au waalimu ulikua na nafuu sana ya kiutendaji.
Lakini sababu ya Pili ni Miundo mbinu ya shule hizi za msingi,shule nyingi haziko vizuri ukianzia majengo,vitabu na walimu,kuna baadhi ya shule hadi leo hii zina mwalimu mmoja au wawili na ikitokea amesafiri shule inaachwa mikononi mwa kaka mkuu wa Shule, hali kama hii imechangia kwa shule nyingi kufanya vibaya kwa sababu wanafunzi hawafundishwi.
Pamoja na Rais Jakaya Kikwete kunukuliwa akisema mwezi huu Serikali itatoa ajira kwa Walimu 28,746 lakini bado kuna upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali idadi ambayo bado ni kubwa kwa kua miongoni mwa idadi hiyo wale wa shule ya msingi watakaoajiriwa ni 14,600 tu ili kukabiliana na upungufu huo.
Tatizo kubwa lililopo hivi sasa ni mgawanyo wa walimu kulingana na shule,Wakati baadhi ya shule zina upungufu mkubwa wa walimu shule zingine zina walimu wengi mpaka wa ziada na hasa shule za mijini hali hii inasababishwa na sababu ya miundo mbinu na mazingira ya kufanyia kazi ambayo siyo rafiki kwa mwalimu kufanya kazi.
Kila binadamu anapenda kuishi vizuri na hasa anapokua amesoma vizuri,kumpangia mwalimu katika shule ambayo haina maji wala umeme na mshahara wake ili kuupata ni lazima afunge safari ni miongoni mwa sababu zinazowafanya walimu kutokwenda kwenye vituo walivyopangiwa au kuacha kazi muda mfupi baada ya kuripoti kwenye shule hizo walizopangiwa na hasa wanapofananisha maisha ya walimu wenzao wa mjini nay a kwao na hivyo kukata tama.
Na sababu ya mwisho ni kukosekana kwa morali miongoni mwa walimu na hasa baada ya Serikali kushindwa kusikiliza malalamiko yao na kuboresha mishahara yao hali hii ndio iliyochangia pia matokeo mabaya ya darasa la Saba kwa sababu walimu hawajitumi ipasavyo na wamekata tama,kwa hiyo pamoja na juhudi za Serikali kuongeza walimu ili kuziba pengo la ikama bado haitakua muarobaini wa wanafunzi kufeli ikiwa walimu hawa hawataboreshewa maslahi yao.
Ki ukweli Walimu hawajitumi kabisa wamechoka na wengi wanasikika wakisema hivyo na ndio maana kuna tofauti kubwa kati ya matokeo ya Shule za Serikali na za binafsi,mbona shule binafsi wamefaulisha sana? Jibu ni rahisi tu wanaifurahia kazi yao na wanajituma kwa sababu mazingira ya kazi ni mazuri ukilinganisha na shule za serikalini.
Hakuna Sekta ya hatari ikilega lega kama sekta ya Elimu na hasa kwenye shule ya msingi kwa sababu ndio kwenye msingi wa kada zingine zote lakini kwa bahati mbaya sana walimu wamesahaulika na hasa wa vijijini mazingira ya kufanyia kazi sio rafiki kabisa kuanzia miundo mbinu na maslahi ya walimu hawa.
Ni lazima Serikali na hasa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha zinatengeneza mazingira mazuri ya walimu kufanya kazi ikiwa ni pamoja na vivutio kwa walimu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu,hivi ni mwalimu gani asiyependa kukaa nyumba yenye umeme na maji na akaangalia Televisheni na kujifunza mambo ya dunia ili akawaongezee wanafunzi elimu ya ziada?
Ni mwalimu gani atakua na furaha kwa kuyasikia au kuyaona haya kwa mwalimu mwenzie anapokwenda mjini kuchukua mshahara?
Kwa mfano unapompokea mwalimu mpya anayekwenda kuripoti akakuta nyuma nzuri ina maji kama umeme wa Gridi au Jenereta haupo basi kuna umeme wa jua (Solar),ameandaliwa shamba la heka moja au mbili ambazo tayari zimelimwa na kupandwa halafu ametengenezewa utaratibu mzuri wa kupata mshahara wake kwa wakati hata kwa kutumia Benki zinazotembea “Mobile Bank” ikiwa ni pamoja na kuweza kukopesheka mwalimu huyu hawezi kukimbia kutoka kwenye kituo chake cha kwanza cha kazi kwa sababu ameandaliwa mazingira mazuri ya kazi na hili linawezekana.
Mambo kama haya ndio yanayowajengea Walimu morali ya kufundisha na hivyo kufaulisha watoto kwenye mitihani ya mwisho hakuna kitu kingine,hata kama Serikali itaajiri walimu na kuziba pengo kwa asilimia Mia Moja bado wanafunzi wataendelea kufeli ikiwa maslahi yao hayata tazamwa upya lakini pia hakutakua na usawa katika mgawanyo wa ikama kwa maana ya kila shule kuwa na idadi inayohitajika ya walimu wenye sifa,haiwezekani shule ya mjini yenye wanafunzi 600 au 700 iwe na walimu 20 mpaka 30 wakati shule kama hiyo kijijini iwe na walimu Wawili au Watano halafu utarajie wanafunzi wafaulu.
Ni lazima Serikali ijipange na kuangalia maslahi ya Walimu na Miundo mbinu yake vinginevyo tusitarajie miujiza kuboresha elimu yetu,tutaendelea kutengeneza kizazi cha ma mbumbumbu kwa sababu ya kudharau sekta hii muhimu,mfano mdogo tu Katika Mkoa wa Morogoro Wilaya ya Morogoro Vijiji kati ya Wanafunzi 6777 waliofanya mtihani ni wanafunzi 2729 tu waliofaulu sawa na asilimia 40.
Wilaya ya Kilosa walifanya mtihani wanafunzi 11939 na ni wanafunzi 6168 tu ndio waliofaulu sawa na asilimia 52,Mvomero wanafunzi waliofaulu ni 4013 kati ya 6555 sawa na asilimia 61,Ulanga waliofanya mtihani ni 5276 na waliofaulu ni 3555 sawa na asilimia 67 wakati Manispaa ya Morogoro ndio iliyofanya vizuri ikifaulisha wanafunzi 5308 kati ya 6059 sawa na asilimia 88.
Kwa ufupi kwa Mkoa mzima wa Morogoro kati ya wanafunzi 45,773 waliofanya mtihani ni wanafunzi 27798 tu sawa na asilimia 61 ndio waliofaulu
Kwa mfano huo mdogo hizo shule za Kata ambazo zilitarajiwa kupokea wanafunzi hawa zitawafundisha kina nani ikiwa wanafunzi 17,975 wamefeli kujiunga na kidato cha Kwanza? Huu ni mfano mdogo tu wa Mkoa wa Morogoro je hali ikoje kwenye maeneo mengine nchini? Tujipange.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment