18 January 2013

Bodi TANAPA sasa kuburuzwa mahakamani


Na Daud Magesa, Mwanza

WANANCHI wa vijijji saba vya kata mbalimbali, katika Wilaya
ya Serengeti, mkoani Mara, wanakusudia kuiburuza Mahakamani
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi 
za Taifa (TANAPA), kwa madai ya kupora maeneo yao.


Bodi hiyo inadaiwa kuweka mipaka ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, tofauti na iliyo iliyowekwa mwaka 1968, kinyume cha sheria namba 282 ya hifadhi, hivyo kuwaingilia kwenye maeneo yao na kuwazuia wasiendelee na shughuli zozote.

Pia wananchi hao wanalalamikia vitendo vya askari wa hifadhi hiyo kukamata mifugo yao nje ya hifadhi na kuwatoza fedha sh. 50,000 hadi 100,000 ili waweze kuiachia jambo ambalo ni uonevu.

Akizungumza na gazeti hili jijini Mwanza jana, mwakilishi wa wananchi wa vijiji hivyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sedeko,
Bw. Richard Nyakera, alisema hivi sasa wanawasiliana na
mwanasheria wao Kampuni ya Kabonde na Magoiga Ltd.

“Lengo la kufikisha suala hili kwa wakili wetu ni kuandaa mashtaka ya kuifikisha Bodi ya TANAPA mahakamani, kwa kutunyang'anya ardhi yetu bila utaratibu.

“Tangazo la Serikali namba 235 la mwaka 1968, liliweka mipaka kati ya hifadhi hii na vijiji hivi kwa kuzingatia sheria ya hifadhi namba 282 bila kuathiri mipaka hiyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, mwaka 2008 uongozi wa TANAPA, uliwageuka wananchi na kudai kuhakiki mipaka ya hifadhi hivyo kutengeneza mipaka yao iliyosababisha baadhi ya maeneo katika vijiji hivyo kuingizwa ndani ya hifadhi.

“Kilichofanyika si kilichokuwa kwenye tangazo na hakikuzingatia haki ingawa wananchi walilalamikia kutoshirikishwa...wananchi walizuiwa kuyaendeleza maeneo yao na kuambiwa watalipwa
fidia lakini hadi sasa hawajalipwa.

“Vijiji hivi vilisajiliwa mwaka 1968, TANAPA wamewaingilia wateja wetu katika mipaka yao...hivyo tunaandaa utaratibu wa kisheria kulifikisha suala hili mahkamani ili haki itendeke,”
alisema Stephen Magoiga ambaye ni mmoja mawakili wa
kampuni ya Kabonde & Magoiga.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Msemaji wa TANAPA, Bw. Pascal Shelutete, alidai hakuna mipaka mipya iliyowekwa isipokuwa wao wanasimamia mipaka ya hifadhi iliyowekwa na kutambuliwa kisheria.

“Kama wanakwenda mahakamani ungesubiri ili habari yako uiandike vizuri...sisi TANAPA tunasimamia mipaka ya hifadhi kisheria si jukumu letu kujiongezea mipaka na hakuna biashara kama hiyo,” alisema Bw. Shelutete.

Zaidi ya kaya 1,000 kutoka Vijiji vya Bisalala, Bonchugu, Tamkeli, Mbalibali, Machochwe, Nyamakenda na Mirenga, vilivyopo katika Kata za Sedeko, Nyansulura, Machochwe na Mbalibali, zinadai kunyang’anywa maeneo yao na TANAPA bila utaratibu pamoja
na kuwazuia wasiyaendeleze.


No comments:

Post a Comment