18 January 2013

TIC 'yakalia kuti kavu' kwa Kamati ya Zitto



Mariam Mziwanda na Rehema Maigala

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imetoa siku moja kwa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),  kuandika barua ya ufafanuzi juu ya uwekezaji katika mkataba wa  Star Media.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe, aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kueleza madhara ya mkataba huo kwa Taifa.

Alisema mkataba huo ambao wabia wake wakuu ni Shirika la Utangazaji nchini (TBC), SDTV na kampuni moja ya kichina umekuwa na mkanganyiko katika malipo ya leseni.

“Mkataba huu, wabia wakubwa ni TBC kwa asilimia 35, SDTV asilimia tatu na kampuni ya kichina asilimia 62, kibaya zaidi mwenye mkataba wa uwekezaji ni TIC.

“TIC ilisamehe malipo ya mtaji kwa kampuni ya kichina na kusamehe kiholela malipo ya leseni kwa TBC, mtaji wa uendeshaji Star Media ulikuwa dola za Marekani milioni moja ambayo kila mdau wake alitakiwa kuchangia lakini kampuni ya kichina
ilikwepa kwa madai ya kusamehewa na TIC,” alisema.

Aliongeza kuwa, TBC ambayo imelipia dola za Marekani 400,000 katika mtaji huo bila kuwepo leseni ya malipo kwa mujibu wa maelekezo ya TIC, pia imeelekezwa malipo hayo yanaingia
katika mtaji.

Bw. Kabwe alisema, TBC limerejeshwa mikononi kwa wananchi ili kulinusuru kutokana na hali mbaya ya uendeshaji.

“Shirika hili halina vifaa na eneo la kazi linalokidhi mahitaji ya huduma bora kwa jamii kutokana na bajeti ndogo iliyopo hivyo kamati imetoa maelekezo ya kuhakikisha linajiondoa katika
mfumo wa matangazo,” alisema.

Aliongeza kuwa, maelekezo hayo yataliwezesha shirika hilo kuondoka katika ushindani wa kibiashara ifikapo Julai mwaka huu na kuziachia kampuni binafsi katika ushindani wa matangazo.

“TBC ina hali mbaya kwa sasa, kamati tumeona ili kuinusuru iendelee kutoa huduma kwa jamii, linatakiwa kurudishwa
mkononi mwa wananchi, pato lao litategemea zaidi huduma za malipo ya king'amuzi...kila mteja atatakiwa kutoa sh.1,000 
kwa ajili ya kuchangia,” alisema Bw. Kabwe.

Alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli na nchini (TPDC), limeshindwa kufuata maagizo yaliyotolewa na Bunge kwa kutopeleka pesa wizarani badala yake zitumike kwa ajili
ya mafunzo na matumizi ya shirika.

Aliongeza kuwa, shirika hilo linashindwa kujiendesha lenyewe kwa sababu ya kukosa pesa wakti Bunge liliagiza asimilia 50 ya mapato yake yapelekwe kwenye mfuko ambao utawanufaisha vijana wa Kitanzania katika mafunzo kwa wanaohitaji kusomea fani hiyo.

“Asilimia nyingine 50 ilikuwa ya matumizi yao pamoja na kujilipa mishahara, kupeleka pesa zote serikalini kunachangia shirika lishindwe kujiendesha lenyewe na ndio maana akuna ajira mpya zinazotoka mbali ya kuwepo uhaba wa wafanyakazi,” alisema.

Alisema pia walitoa maelekezo juu ya mkataba wa bomba la gesi la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili uwanufaishe wananchi na kuwataka wakague mikataba ya mafuta mara kwa mara.

Bw. Kabwe alisema, shirika hilo linatakiwa kufuata Sheria ya Mashirika ya Umma hivyo baada siku tatu, wawasilishe orodha ya utekelezaji wa maagizo ya wabunge ambayo iambatane na orodha kamili ya wanafunzi ambao tayari wameanza kunufaika na mfuko.

No comments:

Post a Comment