03 December 2012

Viongozi jengeni tabia ya kutoa misaada-Meya



Na David John.

NAIBU Meya wa Jiji la Dar es Salaam Bw.Abdalah Chaurembo amewataka viongozi mbalimbali nchini kujenga tabia ya kutoa misaada katika vikundi ili kuinua kipato cha wananchi.

Wito huo ameutoa Dar es salaam jana wakati akikabidhi mikopo ya fedha za mitaji kwa vikundi saba vilivyopo kata ya Mbagala Charambe kwa lengo la kuinua vipato vyao.

Alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi kutoa misaada  ya fedha kwa mtu mmoja mmoja hali ambayo inachelewesha upatikanaji wa maendeleo ya jumla.

"Nawaomba viongozi wezangu kuchangia mitaji kupitia vikundi ili kuwezesha watu wengi kunufaika na misaada hiyo pamoja na kuwezesha kuinua vipato vyao na uchumi wa Taifa,"alisema

Bw.Chaurembo aliwataka wananchi kuona umuhimu wa kujiunga kwenye vikundi ili kuweza kupata fursa za kupata mikopo kwa urahisi kuliko kujitenga na kufanya jambo pasipo mashirikiano.

Naibu Meya huyo alitoa zaidi ya sh.milioni 2 kwa vikundi hivyo na kusema kuwa fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

"Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vikundi kwa lengo la kujipatia fedha kwa ajili ya mambo yao ya anasa,kwa kufanya hivyo hakika hatutafikia malengo ya kujikwamua na umasikini tulionao,"alisema

Kwaupande wake mmoja wa wanavikundi hao waliopatiwa mikopo hiyo, Bi.Zena Said alihaidi kwenda kutumia fedha hizo kama ilivyokusudiwa na kuwashauri wanakikundi wenzake kuzingatia malengo hayo.

Alisema ni jambo la kushukuru kama watu wanajitokeza na kusaidia, hivyo inatakiwa kuonyesha jitihada za kuhakikisha kile unachopewa kinafanya kazi iliyokusudiwa.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Temeke Bw.Robart Kilenge aliwaasa wanavikundi hao kutumia fursa hizo wanazozipata ili kukuza mitaji yao kwakufanya biashara kwa ufanisi na malengo.





No comments:

Post a Comment