03 December 2012

CHADEMA kutoa taarifa za mauaji mikutanoni


Na Goodluck Hongo

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kitatoa taarifa yake siku chache zijazo juu ya hatua za kuchukua baada ya kukosa majibu kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na mauaji ya raia yanayotokea katika mikutano yake.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt.Wilbroad Slaa wakati akizungumza na wajumbe na viongozi wa mkutano mkuu wa jimbo la Kinondoni wakati wa ziara yake ya kukagua uhai wa chama hicho katika Mkoa huo.

Alisema kwa sasa hali ni mbaya kwa raia kutokana na mauaji mengi kutokea na kukosa haki katika maswala yao mbalimbali, lakini hakuna kauli zozote zilizotolewa juu ya kuwachukulia hatua viongozi ambao wanasababisha mauaji hayo wakiwemo Makamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro na Iringa.

"Hakuna majibu kutoka kwa rais juu ya barua tuliyomwandikia, ambapo hadi leo hajajibu, sasa siku chache zijazo kamati kuu itakaa na kujadili hilo na tutatoa taarifa zetu juu ya hatua za kuchukua, kwani Chadema haikurupuki inakwenda hatua kwa hatua,"alisema.

Alisema Chadema si chama cha wanaharakati, kwani kipindi hiko kimeshapita na kwamba sasa kinakwenda kushika dola, lakini tatizo kubwa kwa sasa ni migogoro ya viongozi katika ngazi za chini.

"Hivi wewe mwenyekiti watu wako wa jimbo lako wanajua kama leo kuna kikao, lakini unawatafuta kwa simu hivi utawaambia nini wananchi wa jimbo hili ili wawachague na kuwapa uongozi,"?alihoji 

Alisema badala ya kujadili uhai wa chama katika eneo hilo wanajadili migogoro iliyopo, hivyo badala ya kujenga chama badala yake kunakuwepo na makundi ambapo wengine ni mamluki kutoka vyama vingine ambavyo kazi yao ni kuweka upinzani ili chama  kisiendelee.

Alisema kwa sasa kasi ya Chadema ni kubwa, hivyo  katiba ndio inatakayomuondoa mtu na si vinginevyo na kutoa lawama kwake kuwa amewafukuza wakati wameshindwa kufuata katiba ya chama na inatamka nini juu ya viongozi wa Chadema na majukumu yao na mipaka yake.

Alisema  yeye alivyokosa kwenda Ikulu katika uchaguzi mkuu uliopita aliapa kuwa kazi yake kubwa itakuwa kuimarisha Chama na kukagua uhai wa chama katika maeneo yote na hiyo ndiyo anayoifanya sasa na kuwataka viongozi hao kuweka mshikamano na kuondoa tofauti zao ili waweze kushinda viti vingi katika uchaguzi ujao. 



No comments:

Post a Comment