30 November 2012

Tuwasaidie yatima kielimu, kuboresha maisha yao



KITANDA usichokilalia, huwezi kujua kunguni wake, shida na mateso wanayopata watoto waishio katika mazingira hatarishi na wale wa mitaani ni vigumu kuelezea.


Watoto hawa hawajui leo au kesho watakula nini na hakuna anayehangaika kuwatafutia chakula.

Wanapolala na njaa, hawana wa kumlilia, wakiumwa hakuna wa kumweleza hivyo huendelea na maisha yao hadi wanapopata
nafuu na kupona kabisa.

Watoto hawa hujisikia wapweke na waliokataliwa na ndugu zao, Serikali na jamii kwa ujumla.

Idadi kubwa ya watoto hawa, umri wao unaanzia miaka mwili hadi 10 ambayo kimsingi hawajui kujitegemea, njaa ikiuma wanalia na kushindwa kujieleza.

Kitanda chao ni barabarani na wengine mitaroni, baridi yote ya usiku na jua la mchana ni lao, hawajui kubadilisha nguo, zile walizovaa wiki iliyopita hadi leo hazijatoka mwilini.

Tumezoe kuwaona watoto wenye wazazi wakitoka nyumbani asubuhi na kurudi nyumbani kwao jioni.

Watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi, wakitoka walipoamkia hawajui watalala wapi.

Jamii imesahau kuwa watoto hawa ni sawa na wao, wanasikia njaa, baridi na maumivu sawa na wenzao lakini nani anashughulika nao?

Sisi tunasema kuwa, watoto hawa hawakuchagua kuwa yatima na kuishi mitaani, hawakuchagua kufiwa na wazazi wao, wamejikuta  wapo mitaani na hawana la kufanya kama watoto wetu walivyojikuta wakiwa mikononi mwetu na wanapata kila kitu.

Waswahili wanasema, kinga ni bora kuliko tiba. Mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs na yale ya kimataifa kama UNICEF na Serikali, wanashughulikia tatizo la watoto hawa wakiwa tayari mitaani.

Jambo la msingi, nguvu inayotumika kuwasaidia watoto hawa ingepaswa kuelekezwa kwenye kinga ili kutibu tatizo hilo kabisa.

Sababu moja wapo inayochangia ongezeko la yatima na watoto waishio mazingira hatarishi ni migogoro isiyokwisha katika ndoa.

Hatua za haraka zinahitajika ili kupunguza au kumaliza tatizo la watoto wa mitaani na yatima kwa kuwaunganisha na walezi
pamoja na ndugu zao ambao tunaamini wapo.

Umefika wakati wa Serikali kuhakikisha tatizo la watoto wa mitaani linapatiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwa ni pamoja na kuwakusanya na kuwapeleka shule za msingi, sekondari na vyuoni hasa katika  ufundi ili kuwawekea msingi mzuri kwa maisha yao.

No comments:

Post a Comment