30 November 2012

Tumetumia dola milioni 100 kusaidia maendeleo -Shirika


Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Plan International, limetumia zaidi ya dola za Marekani milioni 100, katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Nigel Chapman, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Bodi ya shirika hilo kufanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali waliyoifadhili.

Alisema hivi sasa wamepanga kutumia dola za Marekani milioni 65 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwenye miradi ya maendeleo.

“Miradi hii itatekelezwa katika maeneo yenye wakazi wengi wenye kipato kidogo na mikoa ya pembezoni nchini, shirika hili limekuwa likifanya kazi nchini kwa zaidi ya miaka 20.

“Kazi kubwa tunayofanya ni kusaidia watoto walio katika mazingira magumu na jamii ya watu masikini ili iweze kupata huduma za afya, elimu, maji safi na salama, hadi sasa watu milioni 1.6 wamefaidika kutokana na programu zetu,” alisema.

Chapman aliongeza kuwa, shirika hilo limekuwa likisaidiana na mashirika mengine kuanzisha Vyama vya Kuweka na Kutoa Mikopo Vijijini (VLSAs), ili waweze kukopa na kuanzisha biashara.

“Kwa sasa kuna vikundi zaidi ya 4,000 vya VLSAs, ambavyo vimeanzishwa nchini kote vyenye wanachama zaidi ya 80,000, wengi wao ni wanawake,” alisema Chapman.

Chapman aliongeza kuwa, shirika hilo limekuwa likiwahusisha watoto katika VSLA ili kuwafanya waweze kuwa na utamaduni
wa kuweka akiba wakimwemo vijana.

Alisema idadi ya klabu za akiba za watoto zimeongezeka na
kufikia 300 ambapo watoto 9,000 wamejiunga.

“Watoto kuhusishwa katika VSLA, inasaidia wawe na utamduni
wa kuweka akiba miongoni na vijana kujifunza menejimenti ya fedha katika hatua za awali katika maisha yao,” alisema.

Aliongeza kuwa, shirika hilo linaisaidia jamii katika miradi ya
usafi ambayo inawafanya wananchi kukataa uchafu kwa sababu
una madhara kiafya ambapo miradi hiyo imeanzishwa katika
zaidi ya vijiji 100.

Shirika hilo limekuwa likiisaidia Serikali kutengeneza sera za kupinga matukio ya unyanyasaji watoto hasa mimba za utotoni
na ajira ambapo hali hiyo hupunguza kesi za ukatili wa kijinsia.

Pia shirika hilo linapigia debe utaratibu wa kujifunza kwa watoto kabla ya kuanza shule unaojulikana kama “Maandalizi ya watoto
na Maendeleo”, wenye lengo la kuwaandaa na kuwapa msingi
imara wa kielimu.

Alisema hilo ni shirika kongwe ambalo lilianzishwa zaidi ya miaka 75 iliyopita na linafanya kazi katika nchi zinazoendelea 50 barani Afrika, Asia na Amerika kwa lengo la kulinda haki za watoto na kuwaondoa mamilioni ya watoto kwenye umaskini.

Nchini Tanzania, shirika hilo lilianza kufanya kazi mwaka 1991, katika Wilaya saba zilizo katika mikoa mitano ambazo ni Ilala (Dar es Salaam), Kisaware na Kibaha (Pwani), Ilemela na Nyamagana (Mwanza), Geita na Nyang’hwale (Geita).

No comments:

Post a Comment