30 November 2012

Avunjika mguu, mbwa akimbia na mfupa wake



Na Thomas Kiani, Singida

MKAZI wa Mtaa wa Murumba, Kijiji cha Munyu, Kata ya Irisya, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Bw. Yahaya Jumanne (30), amevunjika mguu wa kushoto baada ya kupata ajali ya pikipiki
na mfupa wake kuokotwa na mbwa.


Akizungumza na gazeti hili, mfanyabiashara maarufu katika kata hiyo, Bw. Ramadhani Mudia, alisema Bw. Jumanne na mwenzake Bw. Mohamed Athumani (32), walifika nyumbani kwake saa tatu usiku na kukodisha pikipiki yake (CD 250).

Alisema pikipiki hiyo walitaka kuikodi kwa kwa sh. 100,000 ili iwafikishe Singida Mjini wakidai wanakwenda kufuatilia fedha
zao na ilikuwa ikiendeshwa na Bw. Jumanne.

“Binafsi niliwakatalia sana kwa sababu ilikuwa usiku na walikuwa wamelewa hivyo niliamini hawawezi kuimiliki barabarani lakini waliniomba sana, nililazimika kuwapa bila kuchukua fedha zao
bali niliwaambia wairudishe ikiwa salama,” alisema Bw. Mudia.

Kwa upande wake, Bw. Athumani ambaye alikuwa na Bw. Jumanne, alisema walipata ajali hiyo baada ya pikipiki hiyo kuruka kwenye tuta na kuanguka katika eneo la TTCL.

“Kimsingi tulikuwa katika mwendo kasi, tulifika Sindida Mjini salama na ajali ilitupata waakati tukirudi, sote tulianguka chini, mwenzangu mfupa wake wa mguu wa kushoto ulitoka.


“Mimi nilivunjika mkono wa kulia ambao ndio niliangukia baada
ya ajali, wasamaria walifika eneo la tukio na kutukimbiza Hospitali ya Mkoa ambayo ilikuwa karibu na eneo la ajali,” alisema.

Aliongeza kuwa, baada ya kufikishwa hospitali, madaktari wa
zamu ambao waliwapokea, waligundua Bw. Jumanne hakuwa
na mfupa katika mguu wake wa kushoto hivyo waliamua
kuufuatilia katika eneo la tukio.

“Walipofika eneo la tukio walikuta umeokotwa na umbwa ambaye aliuachia baada ya kumdhibiti, waliuchukua na kuuhifadhi katika mfuko wa plastiki,” alisema Bw. Athumani.

Habari zaidi zinadai kuwa, Bw. Jumanne alikimbizwa Hospitali
ya  KCMC Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi
ambapo Bw. Athumani alifungwa bendeji gumu (POP), na kupewa ruhusa ya kurudi nyumbani.

No comments:

Post a Comment