30 November 2012

Ole Naiko apewa tuzo ya utumishi bora serikalini


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bw. Emmanuel Ole Naiko, amepewa tuzo ya ushindi wa kwanza ya utumishi bora wa umma kutokana na juhudi zake
za kusaidia ukuaji wa sekta binafsi nchini.


Tuzo hiyo ilitolewa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni binafsi nchini (CEO Roundtable of Tanzania), katika sherehe iliyofanyika Dar es Salaam juzi.

Akitoa tuzo hiyo, Mwenyekiti wa umoja huo, Ali Mufuruki, alisema kuwa Bw. Ole Naiko amepewa heshima hiyo kutokana na rekodi yake mahiri alipokuwa serikalini kama mtetezi mkubwa wa sekta
ya binafsi ili ishike nafasi kama injini ya ukuaji uchumi wa nchi.

“Kutokana na jitihada zake, Serikali iliweka sera na kanuni nyingi ambazo zilisaidia kuvutia uwekezaji nchini kutoka kampuni za nje na ndani,” alisema Mufuruki wakati akitoa tuzo hiyo.

Kwa upande wake, Bw. Ole Naiko aliushukuru umoja huo kwa kutambua mchango wake na kumtunuku tuzo  maalumu ambayo
imetolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu.

“Hii ni tuzo yenye thamani kubwa kwangu, daimua nashukuru fursa  nyingi nilizopewa kulitumikia Taifa langu ambazo zimekuwa za pekee na zenye changamoto nyingi,” alisema.

Aliongeza kuwa, akiwa Mhandisi mwenye umri mdogo miaka ya 1980, alipata heshima kubwa ya kuteuliwa kuwa Meneja Mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Buckreaf, uliopo wilayani Geita ambao ulikuwa unamilikiwa na Serikali.

“Nilisimamia shughuli za mgodi huu tangu ulipoanza hadi tukaanza kuzalisha dhahabu mfululizo na kuipatia nchi yetu fedha nyingi za kigeni. Hadi naondoka katika mgodi huu mwaka 1989, bado ulikuwa unazalisha dhahabu,” alisema Bw. Ole Naiko.

Alisema baada ya kutoka katika mgodi huo, alijiunga na Taasisi ya Kukuza Uwekezaji (Investment Promotion Centre) ilipoanzishwa
na Serikali mwaka 1990, kabla ya kugeuzwa kuwa TIC.

Aliongeza kuwa, akiwa TIC, alifanya kazi miaka mingi  kama Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji na baadaye kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.

Bw. Ole Naiko, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mahusiano ya Serikali kwenye Kampuni binafsi ya African Barrick Gold (ABG), baada ya kustaafu serikalini, alikataa madai ya kuwa viongozi wa zamani wa Serikali walisaini mikataba mibovu katika sekta za madini na gesi.

“Watu wenye fikra hizo potofu, wamesahau kuwa kabla ya mwaka 1998, hatukuwa na mgodi hata mmoja uliokuwa unazalisha dhahabu ni baada ya kipindi hiki ndio Tanzania ikasonga mbele na kuwa moja ya nchi zinazoongoza Afrika kwa kuzalisha dhahabu,” alisema.

Alizitaka sekta binafsi nchini kushirikiana na Serikali kukuza ukuaji wa sekta ya kati katika uchumi wa Tanzania. “Nawaomba mfanye kila liwezekanalo kuisaidia Serikali katika jitihada zake za kuendeleza kada ya kati nchini,” alisema.

No comments:

Post a Comment