19 November 2012
Nimeitoa CCM ICU-Mukama *Asema ilikuwa imepoteza mvuto, mwelekeo *Chiligati aungana naye kusifu safu mpya *Akemea kejeli, Msekwa akabidhi ofisi *Slaa arusha kombora, amtaka JK ulingoni
Mariam Mziwanda na Grace Ndossa
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama, amejivunia mafanikio makubwa aliyokipatia chama hicho kwa kipindi alichoshika wadhifa huo, kwani chama hicho tayari kilikuwa kama 'kimekufa'.
"Baada ya uchaguzi (2010) chama kilikufa, najivunia kurudisha uhai wa chama uliosababisha kuwepo misingi ya maazimio ya mkutano mkuu, kwani bila CCM iliyo hai hakuna ambacho kingetekelezeka," alisema Mukama.
Mukama alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na gazeti hili lililotaka kujua mchango wake ndani ya CCM kwa kipindi alichoshika wadhifa wa Katibu Mkuu.
Alifafanua kuwa wakati anapewa wadhifa huo aliikuta CCM ikiwa haina mwelekeo, kiasi cha kupoteza mvuto miongoni mwa wanachama wake. "Tuwe wawazi, wakati naingia madarakani nilikikuta chama kina hali mbaya, hasa kutokana na makovu ya uchaguzi wa 2010...nimefanyakazi kubwa kurudisha mvuto wa chama," alisema Mukama na kuongeza;
"Hatua hiyo imezaa matunda ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM kuwa wa kidemokrasia na mfano kimataifa kutokana na hamasa mpya waliyokuwa nayo wanachama."
Kuhusiana na safu mpya iliyopewa jukumu la kuongoza CCM, Mukama alisema; "Ni timu nzuri, Kinana ni mzoefu, mtendaji mwadilifu lakini zaidi sifa yake ya ukali itachangia kurudisha sifa ya chama katika maadili kwani CCM ya sasa inahitaji ukali katika kuelekeza uadilifu."
Alisema kuwa kamwe maneno hayawezi kusaidia kukijenga chama hicho kutokana na usugu wa baadhi ya wanachama na mazoea waliyonayo yanayoua sifa ya chama.
"Nashukuru kukiacha chama katika mikono salama kwani safu hiyo ya uongozi ina uzoefu, hahitaji mafunzo katika kuendeleza harakati za mapambano ya kisiasa, bali ni kuingia kazini ili kutekeleza dira ya chama kupitia sera zake kuweza kubadilika kulingana na wakati," alisema.
Kuhusu matumaini yake baada ya uchaguzi uliowezesha kupatikana kwa safu mpya ya uongozi, Mukama alisema wana-CCM watarajie kupata chama imara na kimoja chenye nguvu.
"Lengo la hii safu ni kuvunja makundi na kuwa na chama kimoja chenye nguvu kitakachosaidia kupatikana ushindi mwaka 2015, kutokana na chama kuwa taasisi inayojivunia mabadiliko," alisema.
Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Kapteni John Chiligati, alisema wanajivunia kukiacha chama kwa viongozi hodari, watu safi na wachapa kazi.
"Hii inatufanya kuamini mapindunzi ya kweli yanawezekana ndani ya CCM," alisema na kuongeza kuwa ipi haja ya kutoa elimu kwa vizazi vya sasa hasa kupitia wao ambao wameona nyakati tofauti kupitia chama hicho, kwani hakuna maendeleo bila msimamo wa Ilani ya CCM.
Alisema pamoja na kustaafu kwao, lakini ieleweke kuwa kejeli ni kupungukiwa na hekima. Kuhusu dhana ya kujivua gamba, alisema lengo lilikuwa ni kuondoa dosari na hadhima ya kutokuoneana haya kwa kuwajibiwa wanaodhorotesha chama kwa matendo yao binafsi.
Kwa upande wake aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Pius Msekwa, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu uongozi wake, alisema; "Kwa sasa siwezi kuzungumza nakabidhi ofisi nitafute siku nyingine."
Akizungumzia timu iliyochaguliwa ambayo CCM inajivunia kwa kuitwa ya ushindi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa, alisema; "Sioni kama ni timu mpya kwa ndani ya CCM, labda kwa kuchaguliwa, hivyo si timu ya ushindi.
Akidhibitisha hilo, Dkt. Slaa alianza kuainisha kasoro za baadhi ya viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho, akiwemo Katibu Mkuu mpya, Philip Mangula na Katibu wa Fedha na Uchumi, Zakia Meghji.
Alisema fedha nyingi ambazo chama hicho kilikuwa kikipigia kelele vimemo vyake vilikuwa vikiandikwa na Mangula wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM. Pia aliainisha kile alichoita udhaifu wa utendaji kazi wa Meghji wakati akiwa Waziri wa Fedha.
Alishangazwa na kauli ya Rais kikwete, kuwataka viongozi wa CCM kujibu mapigo ya wapinzani wakati akijua hawana ubavu huo. "Namwalika Rais Kikwete ajitokeze na kujibu tunayoyasema ili mwongo aweze kujulikana, wakati wa EPA tulisema, lakini rais alisema kelele za mlango azimzuii mwenye nyumba kulala," alisema.
Alisema kwa sasa watu duniani wanapigia kura kwa ajili ya kupata maajabu saba ya dunia, huku Tanzania watoto 5,000 kila mwaka akimaliza darasa la saba na kujiunga na sekondari wakiwa hawawezi kusoma na kuandika.
"Aje hadharani ajibu hoja hizi kwani hakuna mwingine wa kutupa majibu hayo," alisema Dkt. Slaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment