Na Zahoro Mlanzi
SIKU moja baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutangaza mapato ya mechi ya watani ya jadi, Simba na Yanga, uongozi wa Yanga, umekuja juu kwa kusema kuna mchezo mchafu umefanyika kutokana na idadi ya watu walioingia kuwa tofauti na mapato yaliyopatikana.
Shirikisho hilo juzi lilitangaza mechi hiyo kuingiza sh. milioni 390.5 kutokana na watazamaji 50,455 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 30,000 ka viti maalum A (VIP A), VIP B sh. 20,000, VIP C sh. 15,000, na sh. 10,00, sh. 7,000 na sh. 5,000 huku kila timu ikipata sh. milioni 93.
Akizungumza Makao Makuu ya timu hiyo, Mitaa ya Twiga na Jangwani, Katibu Mkuu a timu hiyo, Lawrance Mwalusako alisema hawakutarajia kama yangetangazwa mapato madogo kama hayo licha ya kwamba watu walikuwa wengi uwanjani.
"Sio matarajio yetu kusikia kutangazwa mapato madogo kama yale,kwa mfano kiingilio kingekuwa ni sh. 15,000 tu zingepatikana kati ya sh. milioni 600 au 700 lakini viingilio vilikuwa tofauti tofauti sasa iweje mapato yawe madogo," alihoji Mwalusako na kuongeza;
"Hatujaridhishwa na mgao huo na hii inatufanya tuhisi kuwa kuna mchezo mchafu umefanyika na kuna watu wananufaika na timu hizo zinapocheza,".
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kuzungumzia hilo alisema, wanafanya kazi kwa maandishi na sio na vyombo vya habari, kama Yanga ina malalamiko yoyote wafuate taratibu kwa kuandika barua.
"Si kila kitu abebeshwe mzigo TFF, Ligi inaongozwa na Kamati ya Ligi hivyo masuala mengine ni vizuri wakatafutwa wahusika kuzungumzia hilo,". alisema Osiah.
Wakati huohuo, Yanga imeiomba TFF ichunguze kwa umakini mechi yao dhidi ya Simba kwa madai Mwamuzi, Mathew Akrama hakutaka timu hiyo iibuke na ushindi katika mechi hiyo.
Hayo yamezungumzwa na Katibu wa Yanga, Mwalusako wakati akizungumzia mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika mechi hiyo.
Alisema mwamuzi huyo pamoja na wasaidizi wake hawakuitendea haki timu yake na hasa rafu ya Haruna Moshi 'Boban' alidai alistahili kupewa kadi nyekundu.
Alisema kutokana na mazingira kama hayo, ni vizuri kabla ya kusubili ripoti ya mwamuzi TFF ikafanya uchunguzi wake na kisha kuwachukulia hatua.
Pia alisema timu yao haitavaa nembo ya mdhamini Vodacom yenye rangi nyekundu na nyeupe mpaka watakapopatiwa rangi mbadala, na hata jezi walizopewa hazina ubora unaotakiwa huku logo iliyowekwa akidai si ya timu hiyo.
Katika hatua nyingine, Mwalusako alisema, timu yao inaondoka jijini Dar es Salaam leo ikiwa na wachezaji 18 kwenda Kagera kwa ndege ambapo Jumapili itaumana na Kagera Sugar.
Alisema mara bada ya kumalizika kwa mechi hiyo, kesho yake watakwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya Jumatano dhidi ya Toto African.
No comments:
Post a Comment