08 October 2012
Walimu 'waisuta' CWT
Zourha Malisa na Kassim Mahege
BAADHI ya walimu jijini Dar es salaam, wamedai kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Chama cha Walimu nchini (CWT), kuwa hawatafanya maadhimisho ya siku ya walimu duniani kote kwa sababu Serikali imeshindwa kuwatimizia madai yao.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Uhuru Wasichana, Bi. Elizabert Chuma, alisema pamoja na walimu shuleni hapo kuwa wanachama wa CWT, siku hiyo wameiadhimisha kwa vitendo.
“Sisi tumeadhimisha siku hii kwa kuendelea kufundisha wanafunzi hivyo hatujaunga mkono tamko la CWT, miaka mitano iliyopita tulikuwa tulikuwa siku hii kwa maandamano.
“Walimu waliopo Dar es salam, walikuwa wakikutana katika eneo maalumu na kufanya maadhimisho lakini baadae utaratibu huu ukaanza kusuasua,” alisema Bi. Chuma.
Akizungumzia suala la mgomo, Bi. Chuma alisema, hauna tija bali jambo la msingi ni kukaa katika meza ya mazungumzo ili kufikia muafaka wa tatizo lililopo kati ya walimu na Serikali.
“Mimi binafsi naamini mgomo hauna tija bali ni muhimu kukaa na Serikali ili kufikia muafaka,” alisema Bi. Chuma.
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu Kata ya Gerezani, Bi. Seraphina Mdamu, alisema wao wameamuwa kuadhimisha siku hiyo wakiwa kazini kwa kuingia madarasani ambapo kata hiyo ina shule saba kati ya hizo za msingi tatu na sekondari nne.
“Walimu wa shule zote wameamua kuadhimisha siku hii kwa kuingia madarasani kufundisha, hatujaona sababu ya kugoma, wapo baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu ambao wanahitaji msaada wetu sasa kama tukigoma nani atawasaidia.
“Wakati mwingine sisi ndio tunawasaidia kuwavusha barabara na kuwavusha katika mashimo sasa tukigoma nani ambaye atajitokeza kuwasaidia,” alisema Bi. Mdamu.
Aliiomba Serikali iwaangalie walimu ambao ambao mazingira yao ya kazi ni magumu kwa kuwaongezea posho ambapo kwa kufanya hivyo itakuwa imewasaidia na kufanya kazi kwa kujituma zaidi.
“Hatuna malipo ya muda wa ziada kwani waakati mwingine tunalzaimika kufanya kazi zaidi ili kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi hasa wenye ulemavu hivyo Serikali ituangalie,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment