08 October 2012
Serengeti Boys 'yanusa' michuano Afrika
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), imefuzu kucheza raundi ya tatu na ya mwisho kwenye michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Vijana baada ya Misri kujitoa.
Serengeti Boys ilikuwa icheze raundi ya pili dhidi ya Misri; mchezo wa kwanza ungepigwa Oktoba 14, mwaka huu Dar es Salaam na ule wa marudiano wiki mbili baadaye jijini Cairo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikiho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema katika raundi ya kwanza Serengeti Boys inayofundishwa na Jakob Michelsen kutoka Denmark ilikuwa icheze na Kenya mwezi uliopita, lakini nchi hiyo ilijitoa katika michuano hiyo ambayo fainali zake zitachezwa Machi, mwakani nchini Morocco.
Alisema Serengeti Boys sasa itacheza raundi ya tatu kwa kumkabili mshindi wa mechi kati ya Zimbabwe na Congo Brazzaville ambapo mechi ya kwanza itachezwa Novemba 18, mwaka huu Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika ugenini wiki mbili baadaye.
Alisema Zimbabwe na Congo Brazzaville zitapambana kati ya Oktoba 12 na 14 mwaka huu, Zimbabwe ikiwa mwenyeji wa mechi ya kwanza wakati ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 26-28, mwaka huu.
Wakati huohuo, Wambura alisema timu hiyo itavunja kambi yake kwa mechi ya kirafiki dhidi ya kikosi cha Yanga cha U-20.
Alisema mechi hiyo itachezwa leo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni na kiingilio kwenye mechi hiyo kitakuwa sh. 2,000 tu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment