08 October 2012
Wana CCM walalamikia rushwa katika uchaguzi
Na Daud Magesa, Mwanza
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiendelea na uchaguzi wa viongozi wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho, vitendo vya rushwa vimezidi kushika kasi mkoani Mwanza.
Chanzo chetu cha habari kutoka kwa wana CCM waliozungumza na gazeti hili, walisema baadhi ya wajumbe wenye dhamana ya kuchagua viongozi husika, wanadaiwa kupokea sh. 5,000 hadi 200,000 za wagombea kulingana na nafasi walizoomba.
Walisema hali hiyo inatokana na wapiga kura wenyewe kuomba rushwa kutoka kwa wagombea wa nafasi mbalimbali.
“Pesa inasambazwa kama njugu tena hadharani, hakuna cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kimsingi tusitegemee kupata vongozi bora,” alisema kada wa chama hicho katika Wilaya ya Ilemela (jina tunalihifadhi).
Alisema nafasi zinazoonekana kuwa na ushindani mkali ni ujumbe wa Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Uenyeviti.
Chanzo hicho kilidai kuwa, Katika Wilaya ya Magu, baadhi ya wapambe wa wagombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, walionekana kupigana vikumbo kila mmoja akihaha kutengeneza mazingira ya mgombea wake kushinda.
Wana CCM hao walidai wakati hayo yakifanya, TAKUKURU mkoani hapa inaonekana iko likizo kwani vitendo hivyo vinafanyika bila wahusika kukamatwa.
Walisema inaonesha jinsi gani uchaguzi wa mwaka huu 2015, utagubikwa na vitendo vya rushwa hali inayoweza kusababisha upatikanaji wa viongozi wasio na sifa pamoja na uwezo wa kutumikia wanachama wa CCM na wananchi.
Waliongeza kuwa, Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ambayo aliitoa kwenye sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM Februari mwaka huu, katika Uwanja wa Kirumba, mjini Mwanza, alisema ndani ya chama hicho kuna viongozi wasio na sifa.
Alisema viongozi hao wanakiathiri chama hicho na kuwataka wana CCM kutowachagua kwani sifa ya uongozi wa kununuliwa unakishushia hadhi chama hicho.
Aliongeza kuwa, vitendo vya rushwa katika chama vinafanywa na wagombea wenye uwezo mdogo kifedha ili waweze kushinda katika chaguzi mbalimbali.
Aliwataka wana CCM kutumia vizuri chaguzi hizo ili kupata viongozi bora wasiokigawa chama, wenye uwezo wa kukisemea ambao jamii haitaguna watakapochaguliwa.
Wakati huo huo, mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Bw. Mashimba Mashimba (55), juzi alijikuta akinyang'anywa kipaza sauti wakati akisalimia wajumbe wa chama hicho wilayani Magu.
Bw. Mashimba alipewa kipaza sauti na Katibu wa CCM wilayani humo, Bi. Neema Adam ili aweze kuwasalimia wajumbe hao lakini Katibu huyo alimnyang'anya kipaza baada ya kutaja kujieleza.
Hali hiyo ilizua miguno kutoka kwa wajumbe ambapo Bw. Mashimba aliwataka wajumbe kuchagua viongozi bora ambao watasaidia kurudisha heshima ya chama hicho kwa jamii.
Aliwataka wajumbe kuchagua viongozi ambao watakiletea heshima chama hicho kauli ambayo ilionekana kumkera Mwenyekiti wa sasa, Bw. Clement Mabina.
Alisema Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, imefanya mambo mengi makubwa ndani na nje ya chama bali yanakosa waelekezaji wazuri.
Kwa siku mbili mfululizo, Bi. Adam hakuweza kupatikana ili kutoa ufafanuzi wa kilichotokea katika mkutano huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment