08 October 2012

Mazishi ya Rugambwa Bukoba kwafurika, wageni wakosa pa kulala



Theonestina Juma na Livinus Feruzi, Bukoba

WAKATI masalia ya mwili wa aliyekuwa Kardinali wa kwanza Afrika, Laurean Rugambwa, yakitarajiwa kuzikwa rasmi leo katika Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Huruma mjini Bukoba, mkoani Kagera, idadi kubwa ya wageni waliofika kushuhudia tukio hilo la kihistoria wamekosa hifadhi katika nyumba za kulala wageni.


Hali hiyo inatokana na idadi ndogo ya hoteli na nyumba za kulala wageni mjini hapa ambapo baadhi yao wamelazimika kuhifadhiwa na watu binafsi ili waweze kushuhudia tukio hilo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.

Kardinali Rugamwa ambaye alizaliwa Julai 12,1912, alizikwa mwaka 1997, katika Kanisa la Kashozi mjini Bukoba.

Akizungumza na gazeti hili, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dkt. Methodius Kilaini, alisema maaandalizi ya tukio hilo yamekamilika lakini tatizo lililopo ni uchache wa maeneo ya kuwalaza wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

“Kimsingi maandalizi yamekamilika ila changamoto iliyopo ni uchache wa nyumba za kulala wageni, tumelazimika kuwaomba watu binafsi watusaidie hifadhi kwa ajili ya wageni wetu.

“Watu waliojitokea kuhifadhi wageni katika nyumba hizo, hawatozi fedha bali wamewapa msaada tu hivyo wanalala bure, idadi ya Maaskofu 12 tayari wamewasili mjini hapa,” alisema.

Askofu Kilaini aliongeza kuwa, kati ya wageni wanaotarajiwa kushiriki tukio hilo ni pamoja na Kardinali Emmanuel Wamala, kutoka nchini Uganda, pamoja na msafara wake.

Alisema mazishi hayo yataambatana na maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwake ambapo shughuli hiyo itaanza saa 3:30 asubuhi kwa ibada ya Misa Takatifu.

Aliongeza kuwa, itaongozwa na Kardinali Wamala na itatanguliwa na maandamano kuanzia Parokia ya Kashozi hadi Kanisa Kuu.

Akizungumzia wasifu wake, alidai Kardinali Rugambwa hakuwa na  ubaguzi wa dini, rangi wala kabila.

Katika tukio hilo, waumini wanatakiwa kuvaa sare zilizotengezwa rasmi kwa ajili ya shughuli hizo ambazo hadi kufikia jana zilikuwa zimekwisha na kilichobaki ni bendera pekee ambazo waumini
walikuwa wakizinunua kwa wingi.

Sare zilizokwisha ni vitenge, fulana na kofia ambapo Mkuu wa Mkoa huo, Kanali mstaafu, Bw. Fabian Massawe, alisema suala zima la usalma limeimarishwa ambapo askari polisi tayari wamesambazwa kila kona ya mji huo.

“Nawahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama ni shwari, wao wajitokeze kwa uwingi kushiriki tukio hili,” alisema.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kutokana na nyumba za wageni kujaa, wengi wao wamelazimika kulala katika Ofisi za Wilaya za Muleba na Missenyi.

Tukio hilo litashindwa kuhudhuriwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye ambaye yupo Roma nchini Italia.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambayo imesainiwa na Bw. Richard Kwitega, kwa niaba ya Katibu Tawala mkoani humo, ilisema Bw. Pinda mbali ya kushiriki mazishi hayo, kesho atatabaruku Kanisa Kuu Jimbo Katoliki mjini Bukoba.


No comments:

Post a Comment