08 October 2012

Utekelezaji miradi ya maendeleo utapunguza umaskini katika jamii


Na Rehema Mohamed

UBUNIFU na upelekeji wa miradi ya maendeleo vijijini ni njia mojawapo ya kukuza uchumi wa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

Miradi hiyo inaweza kuwa ya afya, maji kilimo ambayo inaweza kuleta tija kwa wananchi wa eneo husika kwa kuwajengea uwezo wa kujipatia kipato.

Ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hiyo ni nguzo muhimu katika suala zima la kufanikisha malengo ya mradi husika.

Kama inavyoeleweka kuwa wananchi wengi wa vijiji hutegemea kilimo na shunguli ndogondogo ikiwemo biashara ili kupata fedha za kujikimu.

Asilimia kubwa ya biashara hizo huwa za msimu kwakuwa wananchi wengi wa vijijini hutegemea kuuza mazao ya kilimo wanayoyalima mfano matunda ambayo huyasafirisha hadi mijini.

Kilimo pia, huwa hakina uhakika kutokana na asilimia kubwa ya wakulima wa vijijini hulima kwa kutegemea msimu wa mwaka unavyokwenda ambao wakati mwingine kunakuwepo ukame unaosababisha wapate mazao machache.

Kutokana na hali hiyo, pato la mwananchi huyo na taifa linakuwa haliongezeki kulingana na mahitaji ya wananchi na hatimaye umaskini unaendelea kulitesa Taifa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidugalo cha Kanga kilichopo Wilaya ya Kisarawe, Bw.Athumani Sheli akizungumzia suala hilo anasema juhudi zaidi zinahitajika kutoka kwa
serikali, taasisi na wananchi ili kuondoa hali ngumu
ya maisha miongoni mwa wananchi.

Akitolea mfano katika kijiji anachokiongoza anasema, wananchi wa kijiji hicho wanategemea kilimo cha jembe la mkono ambao hulima mazao mihogo na mahindi kuendesha maisha yao.

Bw.Sheli anasema asilimia kubwa ya mazao hayo hutumika kwa ajili ya chakula ukilinganisha na yanayouzwa mijini.

Anasema wananchi wengine huendesha maisha yao kwa kufanya biashara ndogondogo pamoja na kukata na kuuza mkaa, ama kufanya shughuli za shamba kwa watu wengine walio na uwezo. (vimongwe).

Hata hivyo Bw.Sheli anasema hali ya kilimo kwa sasa kijijini hapo imekuwa ngumu, kutokana na wananchi wengi kutegemea kilimo cha msimu wa majira ya mwaka.

Anasema hali hiyo imefanya wananchi wengi kutokuwa na chakula cha ziada cha kuwawezesha kukiuza mijini ili waweze kupata fedha kwa ajili ya mahitaji mengine.

"Kama tunavyojua, kilimo cha kutegemea majira ya mwaka huwa cha kubahatisha, ukame unapoingia mazao hayamei na hivyo kusababisha wananchi wanakosa chakula inavyostahili," anasema bw.Sheli.

Bw.Sheli anasema kuwa huduma ya maji pia ni changamoto kubwa inayokikabili kijiji hicho ambapo kama yangepatikana kwa wingi wangeweza kuhamia katika kilimo cha umwagiliaji.

Bw.Sheli anasema wananchi wake hutegemea visima vya chini kupata maji ambayo si salama kwa matumizi ya kibinadamu hasa kunywa.

Anasema zamani, kijijini hapo kulikuwa na bwawa kubwa la mradi wa maji ambapo hata hivyo yalikuwa yakitumiwa na wananchi wa vijiji vya jirani kama Mareromango na Boga.

"Kijijini kwetu kulikuwa hakuna koki hata moja ya bomba, licha ya ule mradi wa maji kuanzishwa kijijini kwetu, hii ilituvunja moyo sana na iliendelea hivyo mpaka bwawa lilipo kauka maji "anasema Bw.Sheli.

Anasema sasa hivi maji yaliyobaki katika bwawa hilo hayafai kwa shughuli yoyote, hata kunywa, licha ya jitihada za wananchi kuchimba visima vingi ili kupata maji safi.

"Kwa sasa maji tunachota katika kijiji cha Dunda ambako ni mbali na kwa mtu wa kawaida anahitaji kuwa na pikipiki au baiskeli kufika huko, hii hi changamoto kubwa kwa wananchi wa kijiji hiki,"anasema Bw.Sheli.

Anaongeza "Kijiji changu kina kilometa za mraba 200 kwa mzunguko na idadi ya watu ni kubwa ambao wote tunahitaji maji,".

Akizungumzia shughuli za maendeleo kijijini hapo anasema kwa sasa kijiji hicho hakina mradi wowote, wa maendeleo ukiachia ushuru wanaokusanya kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa
magengeni.

Hata hivyo Bw.Sheli anasema hivi karibuni kijiji hicho kimepelekewa mradi wa kilimo cha mihogo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawa ambao utadumu kwa muda wa miaka mitatu ambao hata hivyo bado haujaanza kutoa matunda.

Anasema mradi huu wa mihogo umeanza Machi mwaka huu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe na unatarajiwa kutumia zaidi ya sh. milioni 100 utakapokamilika.

Anasema kupitia mradi huo, kila mwananchi atalima shamba lake na kupanda mbegu mihogo aina ya Kiroba ambayo ni nzuri kwa chakula.

Anasema katika utekelezaji wa mradi huo, baadhi ya barabara za kijiji hicho zitafanyiwa marekebisho ili magari yaweze kupita kwa urahisi katika kipindi cha uvunaji.

Anasema kupitia mradi huo wananchi wanatarajia kupata mabadiliko ya kiuchumi katika kaya zao kwakua soko la zao hilo pamoja na ulaji wake ni makubwa kwa sasa.

"Wananchi wangu wameupokea kwa hali na wana imani kubwa ya mabadiliko kimaisha kupitia mradi huu kama utafanikiwa, kila mwananchi kwa sasa yupo katika hatua ya kuandaa mashamba,"anasema Bw.Sheli.

Katika mradi huo kijiji kitajengewa mashine ya kumenya mihogo, kutwanga na kusaga pamoja na kupata trekta kubwa la kulimia mashamba.

Anasema pamoja na kupata mradi huo, bado kijiji hicho kinahitaji miradi mingi zaidi ili kuboresha hali za maisha za wananchi na kukuza uchumi wao.

Anasema kuwa miradi kama hiyo kama itapelekwa katika vijiji vingie vya wilaya hiyo, upo uwezekano mkubwa wa kuboresha maisha yao hata ukuwaji wa uchumi wa wilaya yao.

Anasema kuwa upelekaji wa miradi huo, uwende sambamba na usimamizi ili kuhakikisha malengo yanayokusudiwa yanafikiwa.

"Miradi ipo mingi ambayo inaweza kupelekwa vijijini na ikapata mafanikio, unaweza kuwa miradi ya ufugaji, maji na hata kilimo kama huu tunaotarajiwa kuletewa kijijini kwetu,"anasema Bw.Sheli.



No comments:

Post a Comment