08 October 2012
Juhudi zinahitajika kupambana na mila potofu zinazowakandamiza wanawake
Na Agnes Mwaijega
SERA ya maendeleo ya wanawake na jinsia ni mojawapo ya sera zilizoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha kuwa wanawake kwa wanaume wanashiriki katika shughuli za maendeleo.
Sera hiyo imetokana na urekebishwaji wa sera ya awali ya Wanawake katika Maendeleo ya Mwaka 1992 inazingatia jinsia kwa kuangalia mahitaji ya wanaume na wanawake kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba kuna ushirikiano wa kutosha kati yao.
Lengo kuu la sera hiyo ilikuwa ni kusawazizisha tofauti zilizopo kati ya wanaume na wanawake ili kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha kutekeleza majukumu mbalimbali kwa kushirikiana.
Asasi mbalimbali zisizo za kiserikali zimekuwa mstari wa mbele kutoa huduma muhimu za kuleta maendeleo ya jamii kwa kuzingatia sera hiyo.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa sera hiyo wanawake bado wanakabiliwa na vikwazo, matatizo na majukumu mengi ya kifamilia yanayowafanya wabaki nyuma kimaendeleo.
Pamoja na serikali kuridhia mikataba ya kimataifa ya kuondoa aina zote za ubaguzi na kutunga sheria mbalimbali za kulinda haki za raia wakiwamo wanawake, bado sheria hizo hazijaonesha kuwalinda walengwa ipasavyo.
Hii inatokana na wanawake walio wengi kukandamizwa na mila na desturi za jamii zao na wakati mwingine hata kutofahamu sheria husika zilizotungwa kwa ajili ya kuwalinda.
Wanaonekana wazi kwamba hawana uwezo katika utekelezaji wa majukumu fulani na kudharauliwa hali inayosababisha wanawake kuogopa kutoa mawazo yao na hata kushiriki kugombania nyazifa mbalimbali za uongozi kisiasa.
Wanawake wamekuwa mstari wa mbele kwa muda mrefu kuhamasisha na kushirikia kikamilifu katika harakati za kisiasa licha ya kukatishwa tamaa na baadhi ya viongozi kuwa hawawezi.
Hata hivyo ushiriki wao katika ngazi za kisiasa bado ni mdogo kwa sababu ya malezi wanayoyapata katika jamii huwafanya wasijiamini kwa kukosa mbinu na uwezo wa kugombea nafasi hizo.
Matokeo ya chaguzi mbalimbali yanaonesha kuwa uwakilishi wa wanawake wabunge, madiwani, viongozi wa dini ni mdogo ukilinganisha na wanaume.
Kwa mujibu wa tafiti zinaonesha kuwa uwiano wa wanawake na wanaume ni mdogo kutokana na mfumo dume ulitawala kwa muda mrefu nchini.
Utafiti uliofanywa na Asasi ya Sante Globale Development Intergree Tanzania (SGDIT) kwa kufadhiliwa na Shirika la Foundation For Civil Society Dar es Salaam katika Wilaya ya Kinondoni kata ya Mburahati umeonesha kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa kuhakiksha kuwa wanashiriki katika ngazi za maamuzi kwa kushika nyazifa mbalimbali.
Wanaamini kwamba wanaume ndiyo wanapaswa kuwa viongozi na kushiriki kutoa maamuzi jambo ambalo siyo sahihi kwa sababu maendeleo endelevu yanategemea hali nzuri ya usawa wa kijinsia katika jamii.
Mratibu wa asasi hiyo Bi.Lulu Wilson anaelezea kuwa jamii nyingi nchini bado zina mila na desturi mbovu ambazo zinapaswa kurekeishwa ili wanawake waweze kuwa na misingi bora ya kujiamini kuanzia wanapokuwa wadogo.
"Ni vizuri kuzienzi mila na desturi njema na kuachana na zenye athari kubwa kwa mfamo kuwanyima watoto wa kike haki ya elimu na uhuru wa kujiamaini," anasema.
Upatikanaji wa usawa wa kijinsia unategemea ushirikiano wa wanawake wenyewe, wanaume, familia, jamii taasisi za kiserikali na binafsi watakavyojizatiti kutekeleza mikakati mbalimbali ya kufikia malengo ya sera ya maendeleo nchini.
Hata hivyo juhudi za wanawake wenyewe zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuacha kujibagua na kujiona hawawezi kushika nafasi hizo.
Bi.Wilson anaongeza kuwa mbinu sahihi ni jamii kubadili mtazamo hasi dhidi ya wanawake na fikra potofu katika mgawanyo wa kazi, majukumu na rasilimali.
Tafiti nyingi zinaonesha kuwa wanawake wanafanya kazi za nyumbani kwa masaa 16 hadi 18 kwa siku ikiwa ina maana kwamba wana masaa 6 hadi 8 ya kupumzika na kulala tu na kushindwa kushiriki katika shughuli nyingine za maendeleo.
Anasema hali hiyo inasababishwa na mila na desturi zilizojengeka kwenye fikra za wanajamii wengi ambazo zinasababisha wanawake kubebeshwa mzigo mzito na kukosa muda wa kujiendeleza na kuwa na maendeleo.
Anaelezea kuwa ushirikishwaji wa wanawake na wanaume katika maendeleo ya taifa utawezekana endapo mchango wa wanawake utatambuliwa na kuthaminiwa.
"Hii itawezekana kama takwimu za wanawake katika ngazi za uongozi kwa kila ngazi zitaongezeka na kuwa na uwiano sawa," anasema.
Anabainisha kuwa Watoto wa kike na wa kiume wakilelewa katika misingi ya haki na usawa haki za wanawake zitapatikana kwa urahisi katika jamii.
Njia bora itakayosaidia suala hilo kuwa na mafaniko nchini ni jamii nzima kuelimishwa juu ya haki za kisheria na kuzingatia usawa.
Bw.Martin Mmbelwa anasema wanawake wanapaswa kuondoa hofu na woga na kujiona dhaifu mbele ya wanaume ili waweze kutimiza ndoto zao na kufikia malengo.
Anaelezea kuwa pamoja na kuwepo kwa mila potofu katika jamii wanawake wanapaswa kujitjamini, kujiamini na kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii kama, elimu, utawala, siasa na kufanya maamuzi.
"Kama hawatafanya hivi watazidi kuwa tegemezi, kutopiga hatua na kushindwa kabisa kufikia lengo la kusawazisha ubaguzi wa jinsia," anasema.
Kwa upande wa jamii Bw.Mbelwa anaelezea kuwa inapaswa kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa kuanzia katika ngazi ya familia hadi taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment