08 October 2012
Tanzania, Kenya kufanya mkutano wa pamoja Taveta
Na Darlin Said
WIZARA ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki itafanya nkutano wa pamoja baina ya Tanzania na Kenya utakaokuwa unatoa elimu na uhamasishaji wa masuala ya Jumiya ya Afrika Mashariki na ukaguzi wa kituo cha pamoja cha utoaji huduma mpakani Taveta
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilisema kuwa mkutano huo utaanza Oktoba nane hadi tisa mwaka huu.
Taaifa hiyo ilisema, Wizara hiyo imekuwa ikiendeleza zoezi la utoaji wa elimu kwa pamoja mipakani.Hadi sasa imefanya hivyo katika mipaka ya Mutukula na Namanga.
"Wizara za Tanzania na Kenya zinazohusika na Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitafanya mkutano wa pamoja juu ya masuala ya Mtangamano wa Afrika Mashariki katika mpaka wa Holili/Taveta kuanzia Oktoba nane hadi tisa mwaka huu,"alisema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo huo ni mkutano wa pili wa pamoja baina ya Mataifa hayo mawili unaoshirikisha viongozi na wananchi waishio mipakani. Mkutano wa kwanza ulifanyika huko Namanga Februari mwaka huu.
Utoaji elimu na uhamasishaji wa masuala ya Jumuiya hiyo katika mpaka wa Taveta utaongozwa na Mawaziri wa Wizara zinazohusika na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw.Samweli Sitta kwa Tanzania na Bw. Mussa Sirma wa Kenya.
Aidha viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na viongozi wa Mkoa wa Taveta Kenya watashiriki wakiambatana na maofisa wao wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na wananchi.
Kufanyika kwa mikutano hiyo ya pamoja mipakani ni utekelezaji wa agizo la Viongozi Wakuu Jumuiya ya Afrika Mashariki walilolitoa katika mkutano wao wa Kumi na Moja wa kawaida uliofanyika mwezi Novemba 2009 huko Arusha.
Katika Mkutano huo, waliagiza kuwa Baraza la Mawaziri liandae Mpango Kabambe wa Kutoa Elimu kwa Umma ili kujenga mshikamano na undugu miongoni mwa wananchi wa Afrika Mashariki na kuharakisha maendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment