08 October 2012

Mawakala 800 ubungo kupatiwa mafunzo


Na Heri Shaaban

MAWAKALA  800 wa kuhudumia abiria katika kituo Kikuu cha mabasi yaendayo Mikoani Ubungo wanatarajia kupatiwa mafunzo ya kazi zao na Chuo Cha Usafirishaji(NIT).


Mafunzo hayo kwa ajili ya kuwajengea uwezo na ufanisi waweze kuhudumia wateja wanaofika katika kituo hicho  ambao wanasafiri kwenda katika  mikoa jirani na nje ya nchi.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana,Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mabasi Ubungo, Bw.Mohamed Kimaya alisema kuwa kabla chuo hicho cha NIT kutoa mafunzo kiliandika barua yao ambayo gazeti hili imefanikiwa kupata nakala yake,ikielezea kukiomba chama hicho kuwaomba watoa huduma kituoni hapo wapatiwe mafunzo yanayotambulika na Serikali.

Bw.Kimaya alisema kuwa walivyoafiki mapendekezo hayo chama chake kiwaita Wamiliki wa Kampuni za mabasi kuwapa mafunzo mawakala na makondakta ambao wanafanya kazi katika kampuni zao za mabasi.

"Mafunzo hayo yatakuwa yakiendeshwa na NIT kupitia kituo chake cha maendeleo kwa wataalam (CPD),ambapo kinatoa kozi za muda mfupi kwa mawakala waendao mikoani na nchi jirani,"alisema.

Alisema kuwa kozi hizo zinalenga kuongeza ufanisi katika utendaji pia litaweza kuhudumia wateja bila fujo katika kituo hicho kutokana na elimu itakayotolewa na wakufunzi hao.

Alisema kuwa baada washiriki ambao ni mawakala kumaliza mafunzo hayo watapatiwa vyeti kila mmoja, na cheti hicho  ukiacha kazi katika kampuni ya basi unaweza ukakitumia katika kampuni nyingine.

Bw. Kimaya alisema madhumuni ya mafunzo hayo yatakuwa yakilenga sehemu ya huduma kwa wateja,nyaraka muhimu za usafirishaji matumizi ya teknolojia katika sekta ya usafirishaji na huduma ya kwanza kwa wateja.

Alisema kuwa awali mafunzo hayo yalikuwa yakilipiwa sh. 60,000 sasa hivi gharama zimepanda na kufikia sh. 11,0000 kutokana na gharama za uendeshaji.

Baadhi ya mawakala wa kituo hicho walikuwa wakigomea mafunzo hayo wakidai yapo kwa manufaa ya watu binafsi na serikali hawatambui mafunzo hayo.



No comments:

Post a Comment