08 October 2012

Serikali yaanza kutekeleza ahadi za Rais Kikwete



 Na Gladness Mboma

SERIKALI imeanza kutekeleza ahadi ya Rais Jakaya Kikwete juu ya kumaliza tatizo la maji katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kutekeleza miradi ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji.


Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe wakati alipofanya ziara ya kuzindua visima vinne vya maji katika maeneo ya Mburahati,Keko Magurumbasi, Keko Mwanga na Unibini Chang'ombe  vilivyochimbwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete.

Waziri Maghembe alisema uchimbaji wa visima hivyo si mwisho wa kumaliza tatizo la maji, bali malengo ya serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika.

Alisema kuwa malengo ya serikali ifikapo mwaka 2015 wawe wamefanikiwa kupeleka maji vijijini kwa asilimia 60 ma mijiji na asilimia 90 na kusisitiza malengo hayo kutekelezwa mapema.

Alisema kuwa wamechimba kwanza visima hivyo ili kuwaondolea hadha ya maji wananchi wa Dar es Salaam wakati wakiendelea kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa itakayoondoa tatizo hilo la maji nchi nzima pindi itakapokamilika.

Prof. Maghembe alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapindu kuakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama ndani ya vijiji na majiji.

Alisema kuwa serikali ipo katika mipango mbalimbali ya kutekeleza miradi mikubwa mbalimbali ikiwemo ya upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu chini ambayo in aendelea na itakamilika kwa muda uliopangwa.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Bw. Arcard Mutalemwa alisema kuwa kuzinduliwa kwa visima hivyo ni sehemu ya visima 27 vilivyochimbwa na serikali katika maeneo tofauti Dar es Salaam ili kukabiliana na tatizo la maji.

Alisema hiyo ni sehemu ya maagizo yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2010 alipotembelea maeneo mbalimbali jijini kuangalia tatizo la maji na kuagiaza kufanyike jitihada za kila aina ili kuakikisha tatizo la maji linapungua katika maeneo yenye ukosefu ya maji, ambapo walianza na uchimbaji visima huku wananchi wakisubiri miradi mikubwa ya maji.




No comments:

Post a Comment