05 October 2012
Kupata taarifa ni haki ya msingi
Na Salim Nyomolelo
HAKI ya kujua na kupata habari ni muhimu katika kukuza, kuchochea pamoja na kuleta maendeleo katika Taifa.
Kupata habari husaidia pia walengwa kurekebisha mapungufu yao inapotokea walifanya makosa na kukosolewa.
Ili maendeleo yaweze kupatikana kuna haja kwa serikali kuhakikisha kuwa haki ya kupata habari inatekelezwa ili wananchi waweze kutambua miradi iliyotekelezwa na mikakati kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii.
Haki ya kujua nchini inatekelezwa na vyombo vya habari ambapo ndio daraja kati ya wananchi na serikali.
Hata hivyo vyombo vya habari ni daraja kati ya mihimili mitatu ya dola yaani Bunge, Mahakama pamoja Serikali ambapo vinatoa taarifa ya utendaji kazi wake kwa wananchi.
Vyombo vya habari ndio vilivyobeba jukumu kubwa la kuwajulisha wananchi tena kwa wakati kuhusu utendaji kazi wa dola ili kutoa maoni yao baada ya kufikishiwa taarifa.
Wakati huo huo dola hutumia vyombo vya habari kufikisha taarifa mbalimbali za utendaji kazi kwa wananchi katika kuhakikisha kwamba utawala bora unafikiwa kwa wakati.
Kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari nchini, serikali imeweka maafisa habari ambao ndio wasemaji wakuu katika wizara, mashirika ama taasisi za umma na binafsi.
Badala ya kutimiza majukumu yao, wamekuwa wazembe na hawatoi ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanahitajika kufanya hivyo na hasa kama ni kujibu shutuma.
Wanashindwa kutumia nafasi waliyopewa kikamilifu kwa kutupiana mpira kujibu ama kutoa taarifa zinazohitajika.
Kutokana na tabia hizo wanahabari hufanya kazi katika mazingira magumu kwa kutopata taarifa muhimu wanazohitaji kujulisha umma.
Mara nyingi wao ndio wasemaji wa wizara na mashirika licha ya kutojua taarifa mbalimbali zinazohusu mamlaka zao na hiyo inatokana na kutokujua wajibu wao.
Nasema hivyo kwa sababu mara nyingi ninapofuatilia taarifa hasa zinazohusu wizara, wasemaji hao hutoa majibu ya kwamba hawajui na kuahidi kufuatilia.
Huu ni uzembe uliopitiliza, kwani ni wavivu kusoma magazeti, kuangalia na kusikiliza taarifa za habari redioni kujua kinachoendelea .
Moja ya sifa za maafisa habari ni kufuatilia taarifa mbalimbali za habari hasa zinazohusu mamlaka zao pamoja na kuwafikishia wahusika wa idara ili zifanyiwe kazi na kutolewa ufafanuzi pale ambapo itahitajika na sio kubweteka na kushitukizwa pindi waandishi watakapofika kutaka ufafanuzi wa jambo husika.
Miongoni mwa maafisa hawa wanawasababishia mawaziri kuonekana kwamba hawatekelezi majukumu yao kutokana na kushindwa kutoa taarifa muhimu za wizara kwa wananchi waandishi wanapohitaji.
Wizara zinatakiwa kuboresha sekta ya mawasiliano kwa umma pamoja na kuwapa semina za mara kwa mara maafisa habari wake ili waweze kutambua ama kukumbushwa kushirikiana na waandishi.
Hii itasaidia kupunguza usumbufu kwa waandishi pamoja na maafisa habari kutambua wajibu wao ili kuweza kuleta utawala bora kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Ikumbukwe kuwa taarifa hizo si kwa ajili ya vyombo vya habari ila ni kwa ajili ya wananchi kuweza kutambua taarifa za serikali kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara ya 18 ambayo inasisitiza utolewaji wa habari kwa wananchi pamoja na haki ya kujua na kupata taarifa.
Serikali inatakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kwani bila vyombo hivi, ni vigumu kutawalika hasa katika hizi zama utandawazi.
Nchi inatawalika kiurahisi kutokana na waandishi wa habari kutekeleza majukumu yake ipasavyo jambo ambalo linasaidia taarifa za Tanzania kujulikana sehemu nyingi duniani.
Natoa wito kwa serikali na maofisa wa habari wakuu kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari ili kukuza ufanisi wa kazi na jamii kupata taarifa kwa mujibu wa sheria.
Wananchi wanapata taarifa za utendaji kazi kupitia vyombo vya habari na sio mikutano ama matarumbeta, hivyo ni lazima waandishi wathaminiwe na serikali.
Mungu Ibariki Tanzania
snyomo@yahoo.com
0715 654410
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment