05 October 2012

Wizara bado haijapokea tathmini kutoka TOC



Na Amina Athumani

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema inasubiri ripoti ya tathmnini kwa vyama vya michezo kutoka Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambayo mpaka jana ilikuwa bado haijawasilishwa.


Waziri  wa Habari, Fenella Mukangara aliviagiza vyama vyote vya michezo vilivyokuwa ndani ya mchakato wa kutafuta nafasi ya kushiriki michezo ya Olimpiki na vile vilivyoshiriki kuandaa tathmini ya miaka minne iliyopita ili kuangalia maandalizi yao yalivyokuwa na wapi vyama hivyo vilikosea.

Kauli hiyo iliagizwa na Waziri Fenella kupitia Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Leonard Thadeo wakati akiipokea timu ya Tanzania ikitokea jiji la London Uingereza, iliposhiriki mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika Agosti 12 mwaka huu.

Kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo Waziri Fenella aliviagiza vyama vyote vya michezo kupitia TOC kuwasilisha tathmini hizo ambazo walitakiwa kuziandaa katika kipindi cha mwezi mmoja tangu kurejea nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Thadeo alisema mpaka sasa bado hawajapokea tathmini hizo na kwamba wanaisubiri TOC ambayo ndiyo iliyopewa jukumu hilo kuziwasilisha kwa Waziri.

Alisema hata kama TOC wameshindwa kupata tathmini hizo kutoka kwa vyama vya michezo wanatakiwa kutoa taarifa ili Wizara ijue nini cha kufanya.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa TOC, Filbert Bayi alipoulizwa kuzungumzia suala hilo alisema ofisi yake bado haijapokea tathmini yoyote kutoka chama chochote cha michezo.

Kwa upande wa vyama vya michezo vilivyolenga kuandaa tathmini hiyo vimedai serikali haikuchangia katika maandalizi ya nyuma hivvyo wasingeweza kuandaa tathmini hizo.

Tanzania katika michezo ya Olimpiki ilifanikiwa kupeleka wanamichezo saba kupitia mchezo wa riadha, ngumi na kuogelea huku kwa wanamichezo wenye ulemavu tukiwakilishwa na mchezaji mmoja ambapo hakuna mwanamichezo aliyeweza kuitoa nchi kimasomaso.

No comments:

Post a Comment