05 October 2012

Yondan nje ya uwanja wiki mbili


Na Elizabeth Mayemba

BEKI wa Yanga Kelvin Yondan atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili baada ya kubainika kupasuka mfupa wa mguu wakati wa mechi yao na watani zao Simba iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Yondan aliumia mguu baada ya kuchezewa rafu na kiungo wa Simba Haruna Moshi 'Boban' na hivyo kushindwa kurudi tena uwanjani.

Akizungumza Dar es Salaam jana Daktari wa timu ya Yanga, Juma Sufiani alisema Yondan baada ya kupelekwa hospitali na kufanyiwa X-ray ilibainika kuwa mfupa umevunjika hivyo anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili au zaidi kutokana na hali yake itakavyokuwa.

"Yondan aliumia sana kwa ndani na baada ya kufanyiwa vipimo ikagundulika kuwa mfupa wa umevunjika hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili au zaidi ili arejee tena uwanjani na kuanza mazoezi mepesi mepesi," alisema Sufiani.

Alisema wachezaji wengine wanaendelea vizuri isipokuwa walikuwa na majeraha madogo madogo akiwemo Mbuyu Twite ambaye alivimba vidole vya mguuni, lakini hali yake inaendelea vizuri na anaweza kucheza endapo kocha ataamua kumpanga.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabalo alisema kuwa jana jioni akiwa na baadhi ya viongozi walikwenda kumwagalia Yondan hotelini kwake na hali waliyomkutanayo haikuwa nzuri hivyo wakalazimika kumpeleka hospitali.

"Kwakweli baada ya jana kwenda hotelini kwa Yondan tulimkuta bado anaugulia maumivu hivyo tutampeleka hospitali ambako walimpiga X-ray na kugundua tatizo, kama viongozi imetusikitisha sana," alisema Katabalo

Timu ya Yanga jana ilikuwa ikijifua kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar unaotarajiwa kupigwa Jumapili Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

No comments:

Post a Comment