08 October 2012

Mikakati kuboresha afya iongezwe kuongeza uzalishaji mali nchini



Na Raphael Okello

MWAKA huu mfuko wa Bima ya taifa(NHIF) imetimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 ikijivunia kuwafikia
wananchi katika kila Mkoa.


Katika mkoa wa Mara Mfuko wa Bima ya Taifa(NHIF) na mfuko wa afya ya Jamii(CHF) imeendelea kuweka mikakati yake ili kuhakikisha kila mkazi wa mkoa wa Mara anafikiwa.

Mifuko hiyo inalenga kusaidia jamii katika  sekta za umma na binafsi pamoja na makundi yote ya akina mama, wazee na walemavu.

Mkuu wa mkoa wa Mara Bw. John Tupa anasema kuwa sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji
kushughulikiwa na wadau wa afya kupitia mfuko wa NHIF na CHF.

Anasema kuwa serikali ilipitisha sera ya huduma za afya kuchangiwa katika mifuko hiyo na kwamba yale makundi maalum yana utaratibu wake katika kuhakikisha wanapata huduma hizo.

Bw. Tupa anasema kuwa lengo ni kujadiliana ili kuboresha huduma na siyo kutupiana lawama na kutafuta mchawi katika suala la kuboresha huduma za afya.

Anasema ni fursa ya NHIF na CHF kutumia vizuri mifano ya
baadhi ya halmashauri za wilaya mkoani humo ambazo zilitunukiwa tuzo ya usimamizi mzuri wa fedha na kuboresha huduma ili kusaidia kuwavuta wananchi kujiunga na CHF na kupata matibabu kwa njia ya kadi," anasema.

Anasema ni jukumu la viongozi wa NHIF kuwaeleza wananchi kuhusu maeneo ambayo mshiriki mmoja mmoja anaweza kuchangia mfuko ili kuboresha huduma za afya kwa wanachama wake.

Anawataka waratibu wa NHIF na CHF kutumia utalaamu wao katika huduma za matibabu kupitia Mfuko wa afya na kuelimisha umma kufanikisha dhamira ya serikali ya Watanzania kwenye utaratibu wa Bima za Afya.

“Ni ukweli ulio wazi kuwa gharama za matibabu zinapanda kila siku hivyo ni njia pekee ya kumkomboa Mtanzania  kumpa uhakika wa kutibiwa yeye na familia yake kupitia mfumo wa Mfuko wa Afya ya jamii ambao NHIF uko chini yao,” anasema Bw. Tupa.

Anafafanua kuwa CHF ni ndoto ya kila kiongozi katika ngazi zote za serikali na kuwataka wananchi wa mkoa wa Mara kutumia rasilimali ndogo walizonazo za mifugo na mazao wanayozalisha kuboresha afya zao.

Bw.Tupa anafafanua  kuwa mkoa wa Mara ni moja ya mikoa ambayo wananchi wake wanachangamkia fursa za maendeleo kila zinapojitokeza.

Hata hivyo anasema kuwa viongozi na waratibu wa NHIF na CHF
hawajaonesha mwamko katika kuchangamkia fursa ya utaratibu rahisi wa kuchangia matibabu kupitia mfuko wa afya ya jamii(CHF).

Katika kutekeleza hayo takwimu mkoani Mara inaonesha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana kati ya kaya 237,071 ni jumla ya kaya 1,460 tu ndizo zilizojiunga na CHF idadi ambayo ni sawa na asilimia 0.6 ya kaya zote.

Anaeleza kuwa si kweli kwamba wakazi wa mkoa wa Mara  hawana uwezo wa kuchangia shilingi 10,000 kwa kaya ndani ya mwaka mmoja bali tatizo inawezekana ni wananchi kutoelimishwa vya kutosha juu ya  mfuko huo.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo mkoani hapa, hali ya uchangiaji wa mfuko wa Afya ya jamii katika mkoa huu hairidhishi,” anasema Bw.Tupa.

“Kila kiongozi kwa nafasi yake anatakiwa kushauri ni mikakati gani ya kuhakikisha hali hiyo inabadilika ili wananchi wajiunge na Mfuko huo”.

Akitaja baadhi za fursa mkoani Mara, Bw. Tupa anasema kuwa Mkoa umebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa ambapo mazao mbalimbali yanastawi vizuri.

Anaeleza uwepo wa ziwa Victoria ambalo linasaidia shughuli za
uvuvi kuendelea na kuongeza pato kwa wananchi wa mkoa wa Mara.

“Ukizingatia hayo wananchi wa mkoa wa Mara wakati wote wako katika shughuli za uzalishaji kwa njia ya kilimo, uvuvi na  ufugaji,”

“Kazi hizi zitafanywa tu ikiwa afya ya wananchi ni njema na mapato hayo bado yanawawezesha kujiunga na NHIF au CHF” anasema Bw. Tupa.

“Familia yenye maradhi kila wakati inakosa muda mzuri wa kuzalisha mali, kila familia ni lazima iwe na uhakika kuwa mmoja wao anapougua wana uwezo wa kwenda kwenye kituo cha matibabu  na kutibiwa hata kama hana fedha mfukoni,” anaeleza.

“Uhakika huu wa matibabu utapatikana tu iwapo wananchi wengi
watajiunga na CHF na wakishirikishwa katika usimamizi wa huduma kupitia Bodi za afya”.

Anaiomba Bodi ya NHIF kutafuta njia ya kuwahamasisha wananchi kujiunga na CHF na kuhakikisha kuwa wanapokwenda katika vituo vya afya wanapata huduma zinazostahili.

Aidha  watoa huduma wa mfuko wanatakiwa kutoa  huduma za heshima wananchama wa mfuko kwa kuwa huduma hizo zimelipiwa tayari hivyo watibiwe mapema na kwa haraka.

Lakini pia wanachama wanatakiwa wawe walinzi wa huduma wanazopata hasa pale wanapokutana na  dawa zinazotolewa
na serikali zinauzwa katika maduka ya watu binafsi watoe taarifa kwa vyombo vya usalama ili hatua stahili zichukuliwe.

Lakini pia anawataka watoa huduma kufanya kazi kwa uadilifu na kubaini wanaofanya udanganyifu katika vitambulisho vya matibabu kwa lengo la kuusaidia mfuko kuondokana na gharama zisizostahili.

Anapendekeza kuwa waajiri wahakikishe kuwa wanawaandaa watumishi wanaokaribia kustaafu ili waweze kurejesha vitambulisho vya Mfuko na kufuata utaratibu uliowekwa katika kupata vitambulisho vipya.

Anasema mkakati wa kuboresha Mfuko wa NHIF na CHF mkoani Mara ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila halmashauri inaweka malengo ya uandikishaji wa kaya kujiunga na CHF na taarifa kuwasilishwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa kwa ufuatiliaji zaidi.

Anazitaka halmashauri ambazo ziko nyuma katika mpango huo viongozi wake waweke vipaumbele.

Bw. Tupa anawashauri wabunge na madiwani mkoani kufuatilia taarifa za fedha zitokanazo na mfuko wa CHF ili waweze kujua matumizi yake.

Dkt. Leornad Mitti ni meneja wa Mfuko wa Bima ya Taifa(NHIF) mkoani Mara yeye anasema kuwa Mfuko wa Taifa ya  afya uliundwa kwa sheria ya bunge namba 8 ya mwaka 1999 na utekelezaji wa mpango wake ulianza rasmi julai mwaka 2001 kwa watumishi wa serikali kuu peke yake.

Dkt. Mitti anasema kuwa tangu mwaka 2001 NHIF mkoani Mara imeendelea kuandikisha wanachama na kutoa vitambulisho ambapo jumla ya watumishi 12,581 wa umma sawa na asilimia 87.7 wamekuwa wanachama.

Anasema wanaofaidika na mfuko ni 69,230 ambapo marekebisho ya sheria na.3 ya mwaka 2009 na.2 ya mwaka 2010 yalijumuisha makundi ya madiwani, wastaafu na majeshi ya polisi, magereza, jeshi la zimamoto na uhamiaji.

Anasema  kwa kipindi hicho Mfuko wa taifa ya Bima ya afya mkoani Mara umekusanya zaidi ya sh.36,811,948.14 ambapo ndani ya mwaka mmoja jumla ya kaguzi 13 zimefanyika zikiwa na lengo la kuhakiki taarifa mbalimbali za watumishi.

Kuhusu zoezi la ukusanyaji fomu ya wanachama na usambazaji wa
vitambulisho Dkt. Mitti anasema kuwa jumla ya Fomu 2,903 zimekusanywa ambapo vitambulisho 5,797 vimesambazwa kwa wanachama licha ya baadhi ya watumishi kutojaza fomu zao.

Kuhusu mfuko wa afya ya jamii(CHF) mkoani Mara, Dkt. Mitti anaeleza kuwa ofisi yake inaandaa mafunzo kwa waratibu wa CHF wa wilaya zote ikilenga kepeana taarifa na kubadilishana uzoefu kwa shughuli za CHF.

Anasema mafunzo hayo pia yanalenga kutoa mbinu mpya  na hamasa kwa waratibu katika kuwasajili wanachama wapya.

Pamoja na changamoto zingine Dkt. Mitti anasema kuwa baadhi ya halmashauri mkoani Mara hushindwa kuwasilisha michango ya
madiwani kwenye mfuko wa Bima ya afya kwa mujibu wa sheria.

Anabainisha kuwa ni pamoja na baadhi ya wanachama
wanaokoma utumishi kutorejesha vitambulisho vyao ikiwa ni pamoja na wastaafu, walioacha kazi na waliofariki.

Pia, kuongezeka kwa udanganyifu wa kupata huduma na idadi ndogo ya kaya zinazojiunga na CHF pamoja na baadhi kutumia vitambulisho visivyo vyao.

Dkt. Mitti anaeleza kuwa taarifa za wanachama wa CHF, mapato na matumizi ya fedha za CHF kutoeleweka katika halmashauri sambamba na halmashauri nyingi kushindwa kuomba fedha za TELE kwa TELE kwa kukosa viambatanishi.

Dkt. Mitti anaomba Bodi za Afya za halmashauri ziweke mpango mizuri ya kuboresha huduma za afya kwa kutumia fedha zilizochangwa na wananchi pamoja na kuhakikisha fedha za NHIF na CHF zinarudi vituoni kuboresha huduma.


1 comment:

  1. majira wanashindwa kumili tovuti inayoeleweka? maajabu,makubwa, wani email shida yao ankwita@yahoo.com nishauriane nao kwa kweli inatia wasiwasi

    ReplyDelete