10 September 2012
Wazee CHADEMA wasikitishwa mauaji yanayoendelea nchini
Na Neema Kalaliche
BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limelaani na kusikitishwa kwa kitendo cha mauaji kinachofanywa na vyombo vya dola, hususani Jeshi la Polisi.
Kaimu Katibu wa Baraza la Wazee Taifa, Bw.Erasto Gwota katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam alisema kuwa Jeshi la Polisi linatumia risasi za moto na mabomu kupiga, kutesa na kuua raia wasiokuwa na hatia.
Alisema kuwa baraza hilo linashangazwa na ukimya wa Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, juu ya mauaji yanayojirudia yanayosababishwa na vyombo vya dola na taasisi zingine anazoziongoza.
"Tunatoa wito kwa wazee wastaafu walioiongoza serikali na wazee wa CCM kama wanaitakia mema nchi yetu wamshauri Rais Kikwete ajitokeze ili azungumze na Taifa na achukue hatua kali za kuwaajibisha viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi wanaotoa amri zinazosababisha umwagaji damu kwa raia,"alisema.
Alisema kuwa ukimya wa Rais Kikwete unajenga hisia kuwa mauaji hayo yana baraka kwa viongozi wa serikali na endapo ataendelea kuwa hivyo Baraza la Wazee litaishauri CHADEMA kuwaongoza Watanzania kuchukua hatua kali dhidi yake, serikali na CCM anayoiongoza.
Pia alisema kuwa Baraza hilo linalaani kitendo cha Jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya kikatili ya Mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten Bw.Daudi Mwangosi yaliyotokea katika vurugu za CHADEMA na polisi Septemba 2 mwaka huu.
"Tunalaani vikali kitendo cha Jeshi hilo kutumia nguvu katika kutuliza ghasia na hatimaye kuua au kuwasababishia madhara wananchi wa kawaida wakiwemo wafuasi wa CHADEMA ambao wanakuwa hawana silaha zozote," alisema.
Alisema kuwa Baraza hilo linatambua mpango huu wa kuazisha vurugu pindi inapotokea mikutano ya CHADEMA ina lengo la kukizorotesha chama hicho na kuwafanya wananchi watambue kuwa CHADEMA ni chama cha fujo wakati wao wana lengo la kuwakomboa wananchi katika siasa chafu zinazoendelea.
Alisema kuwa CCM inajaribu kupindisha na kuminya demokrasia kwa hofu kwamba kitaondolewa madarakani katika uchaguzi ujao, hasa kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 kisha uchaguzi mkuu, 2015.
"Hii ndio inapelekea Serikali kutumia mabavu na risasi za moto kuongoza nchi na kuminya haki za raia, jambo linalochangia uvunjifu mkubwa wa amani,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment