10 September 2012
Katibu CCM atimkia ADC
Na Anneth Kagenda
KATIBU wa Siasa na Uenezi Tawi la Tuangoma Mbande Wilaya ya Temeke toka chama cha CCM Bi. Zulfa Adam ameamia Chama Kipya cha Alliance for Democratic Change (ADC) huku akitamba kunogewa na sera na kuahidi kuwashawishi wengine kujiunga na chama hicho.
Hayo aliyasema jana wakati akirudisha kadi ya CCM na kupokea kadi mpya ya ADC mara baada ya uzinduzi wa Tawi Jipya lililozinduliwa na Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke ya chama hicho Bw. Salum Soud, ambapo pia wanachama 91 walijiunga na chama hicho.
Alisema pia aliwahi kukaimu Kata kwa zaidi ya miaka miwili ambapo alisema kuwa baada ya kusikiliza sera za ADC aliridhika nazo na kuona kwamba ni bora kuamia katika chama hicho kutokana na kuona CCM imepoteza mwelekeo, kina mpasuko wa hajabu na kuahidi kuongeza nguvu ili iweze kuwa na wanachama wengi.
Naye Bw. Soud alisema hivi sasa wamelenga kuwaleta wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya kuwafundisha wanachama wao elimu ya ujasiliamali lengo likiwa ni kuwaondoa kwenye lindi la umaskini huku akisema vijana wataweza kujikwamua kutokana na vyama vilivyopo kushindwa kuwajali.
"Tumeanzisha dawati Makao Makuu la wataalamu toka UDSM lengo ni kutoa elimu ya ujasiriamali kwa Watanzania, kuwapatia uwezo mkubwa wa kuwajenga kiuchumi, elimu itakayotolewa kila tawi nchini.
Alisema lengo lingine la chama hicho ni kila tawi ndani ya nchi kuwa na kitegauchumi ambacho wasimamizi watakuwa ni wanachama wenyewe na watabuni miradi mbalimbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment