07 September 2012
UTPC watoa tamko mauaji ya Mwangosi
Esther Macha na Mwajabu Kigaza
UMOJA wa Klabu za Uandishi wa Habari nchini (UTPC), jana umetoa tamko la kuitaka Serikali kuwasimamisha kazi askari polisi waliohusika na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni Channel Ten, mkoani Iringa Bw. Daudi Mwangosi.
Tamko hilo limetolewa Dar es Salaam jana na Rais wa umoja huo, Bw. Keneth Simbaya, wakati akizungumzia msimamo wao dhidi ya mauaji ya Mwangosi, yaliyotokea mikononi mwa polisi kwenye Kijiji cha Nyalolo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Alisema operesheni iliyokuwa ikifanywa na polisi kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni haramu hivyo askari wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanapaswa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao.
“Uchunguzi juu ya mauaji ya mwenzetu ukikamilika, tunaitaka Serikali itangaze matokeo yake kwa umma na kuchukua hatua za kisheria kwa polisi ambao wataguswa na uchungusi huu,” alisema.
Bw. Simbaya aliongeza kuwa, wakati uchunguzi huo ukiendelea Serikali itenge fungu la fedha kwa ajili ya mjane wa Mwangosi na watoto wa marehemu ili waweze kujikimu kimaisha.
Alisema licha ya kutoa tamko hilo, wataendelea kulitaza Jeshi la Polisi kama mdau wa mashaka wanapofanya kazi na waandishi.
“Katika mkutano wetu, tumeridhia kushirikiana na taasisi zingine za haki za binadamu, uwakili na utetezi ili kubaini namna bora ya kuishtaki Serikali kama mwenendo wa suala hili hautaleta tija.
“Katika kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa usalama, tumelitaka Jeshi la Polisi kutoa utaratibu utakaowawezesha wanahabari nchini kufanya kazi kwa usalama bila hofu na dharau,” alisema Bw. Simbaya.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Vyama vya Waandishi wa Habari nchini ambao walihudhuria mkutano huo, walisema lililotolewa halijapewa uzito kutokana na tukio la mauaji husika.
“Hili tamko lilipaswa kupewa uzito mkubwa kulingana na mauaji yenyewe jinsi yalivyokuwa yanatisha hivyo tunapaswa kuzingatia maagizo ya kususia habari za Jeshi la Polisi hadi watakapoona umuhimu wa kukaa meza moja,” alisema Bw. Christopher Nyenyembe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

ki ukweli hili sio tamko bali ni maelekezo tu, najua wanaiogopa serikali yasije yakawa mengine kabisa kwani sasa nchi hii imekuwa sio huru tena kwani ukionekana unafumbua jambo dhidi ya serikali basi unakiona cha mtema kuni.
ReplyDeleteki ukweli hili sio tamko bali ni maelekezo tu, najua wanaiogopa serikali yasije yakawa mengine kabisa kwani sasa nchi hii imekuwa sio huru tena kwani ukionekana unafumbua jambo dhidi ya serikali basi unakiona cha mtema kuni.
ReplyDelete