07 September 2012
TCD, Pinda kujadili machafuko nchini
Na Tumaini Maduhu
KITUO cha Demokrasia nchini (TCD) kimepanga kwenda kumuona Waziri Mkuu, Bw Mizengo Pinga, ili kufanya nae majadiliano juu ya machafuko yaliyosababisha vifo vya watu wasio na hatia katika mikoa ya Arusha, Morogoro na Iringa.
Mwenyekiti wa kituo hicho, Bw. James Mbatia, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kulaani vikali mauaji ya mwandishi wa Kituo cha Televisheni Channel Ten, Daudi Mwangosi kilichotokea hivi karibuni.
Alisema moja ya agenda ya kikao hicho ni kujadili namna bora ya kuondoa machafuko yanayotokea mara kwa mara ambayo yanaligharimu Taifa kwa kupoteza nguvu ya kazi.
“Hoja ya kukutana na Bw. Pinda tayari iko mezani kwangu hivyo naamini tutafikia muafaka na kuhakikisha mambo haya hayatokei tena nchini kwetu,” alisema Bw. Mbatia.
Aliongeza kuwa, inashangaza kuona Watanzania wengi wanapoteza maisha bila sababu za msingi ambapo machafuko, mauji yote yanayotokea nchini ni dalili mbaya ambayo kama itanyamaziwa kimya Taifa haliwzi kufika mbali.
Alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, mwanadamu yeyote hapaswi kuondoa uhai wa mwenzake hivyo Watanzania waache kunyoosheana vidole kutokana na kifo cha mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.
“Tuwe na moyo wa kusubiri matokeo ya tume iliyoundwa ili kujua chanzo cha mauaji ya Mwangosi, kama hatujaridhika na majibu yaliyotoka, tutaamua nini cha kufanya kwa sasa ni mapema kunyoosheana vidole,” alisema.
Bw. Mbatia alisema wameandaa rasimu ya maadili ya utendaji kazi kati ya Serikali na vyama vya siasa nchini ili kuwepo na utendaji wa maadili baina ya pande hizo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment