07 September 2012

Kibamba: Tume ya Haki za Binadamu toeni tamko


Mariam Mziwanda na Peter Mwenda

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imeshauriwa kusimamia haki za Watanzania na kutoa tamko kuhusu kifo cha aliyekuwa mtangazaji wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, kwa kuunda tume ambayo itasaidia kutenda haki.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Bw. Deus Kibamba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kusisitiza kuwa, mbali ya tume hiyo Bunge kupitia Spika wake naye anamamlaka ya kufanya hivyo.

“Sasa tumepata picha kamili kuwa tuna tume na Bunge lisilojiamini, linalosubili maamuzi ya Rais ndio awatendee kazi zao, kifo cha Mwangosi ni cha kikatiba na wanahaki ya kutetea haki za mwandishi huyu,” alisema Bw. Kibamba.

Aliongeza kuwa, jukwaa hilo lipo tayari kutoa elimu ya maandamano kwa jeshi hilo na haki za msingi zinazotakiwa kufuatwa kwani ni wazi kuwa, jeshi hilo limekosa elimu hiyo na kujikuta likivuka mipaka hadi kufikia hatua ya kuua raia wake.

Bw. Kibamba alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anaunda tume ambayo itachunguza mauaji hayo na mapendekezo yake yafanyiwe kazi.

“Tume hii isishirikishe Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye naye anahusika kutokana na mamlaka aliyonayo, ipo haja ya kumsimamisha kazi Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda ili kupisha uchunguzi wa tukio zima,” alisema.

Ametoa wito kwa Serikali kutangaza rasmi uamuzi wa kuchukua jukumu la kuitunza, kusomesha, kulisha na kuhudumia familia ya marehemu Mwangosi kuanzia sasa hadi miaka 20 kwa sababu kifo chake kimesababishwa na bomu la polisi.

No comments:

Post a Comment