07 September 2012
Nape ahadharisha mifarakano ndani ya CCM
Na Wilhelm Mulinda, Mwanza
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Nape Nnauye, amesema vyama vyote vilivyoleta uhuru katika nchi mbalimbali duniani, hujiondoa vyenyewe madarakani kutokana na mifarakano ya wanachama wake.
Bw. Nnauye aliyasema hayo jijini Mwanza jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, kama mifarakano haitakuwepo katika vyama vya upinzani, si rahisi kwa vyama vya upinzani kuingia madarakani.
“Ni vigumu vyama vya upinzani kuchukua dola kwani si rahisi wapinzani kujipenyeza ndani ya CCM ili kuivuruga,” alisema.
Aliongeza kuwa, CCM kinaweza kupenyeza watu wake katika vyama vya upinzani kwani hakuna aliyeanzisha vyama hivyo bali viongozi wake wote wametokea chama tawala.
“Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Laour Party (TLP), Bw. Augustine Mrema na Bw. Mabere Marando ambao hivi sasa ni viongozi wa vyama vya upinzani, kabla ya hapo walikuwa wanachama wa CCM na walifanya kazi katika idara nyeti serikalini,” alisema Bw. Nnauye.
Aliongeza kuwa, CCM itaendelea kuwa madarakani kwa muda mrefu kwa sababu bado inakubalika na wananchi kutokana na msingi mzuri wa uongozi kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Bw. Nnauye alisema suala la kuvuja kwa siri za vikao vya chama ni changamoto kubwa kwa sasa na kudai kuwa, dawa ya tatizo hilo ipo jikoni.
Alisema hivi sasa kuna mtindo wa baadhi ya wafanyabiashara kutamani uongozi ndani ya chama hicho ambapo hata wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, CCM ilikuwa na wafanyabiashara waliomsaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza chama kwa masilahi ya Taifa.
Aliongeza kuwa, wanacholaani sasa ni kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kuingia katika chama hicho na kutumia fedha zao ili kupata uongozi kitendo ambacho hakiwezi kukubalika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

Nape acha kujifariji,CCM kinaenda kufa jumla.
ReplyDeleteJifariji kwa huo mtazamo lakini mabadiliko ni lazima kwa msababu atanzania wa leo si wa kudanganywa na siasa uchwara! M4C!! upo hapo?
ReplyDelete