17 September 2012

Shule sita Mwembe Madafu zapatiwa mapipa 18 ya taka


Na Stella Aron

MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Bw. Wilfred Kipodya, kwa kushirikiana na uongozi wa manispaa hiyo, wamesambaza mapipa 18 ya kuhifadhi taka katika shule sita za msingi zilizopo mtaa huo ili kuboresha mazingira.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaama jana, Bw. Kipodya alisema kila shule ilipata mapipa matatu ambapo mradi huo ulipata ufadhili wa wadau wa mazingira nchini Finland.

Alisema wadau hao walikuja nchini kwa ajili ya mpango wa kuboresha mazingira ambapo mtaa huo ulipendekezwa kuwa wa majaribio kupitia mradi huo.

“Mtaa wangu ulipendekezwa kuwa wa majaribio na wafadhili ambao walifika nchini ili kuboresha mazingira na kupunguza taka zilizozagaa mitaani,” alisema.

Bw. Kipondya alisema hatua hiyo inatokana na wanafunzi kuanza kujifunza mpango wa kuboresha mazingira ambao utawasaidia kuhamasisha suala zima la usafi mitaani.

Alisema mapipa mawili yatawekwa mitaani hivyo kufikia 20 ambapo wananchi wataelimishwa umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kutupa taka katika maeneo maalumu.

Bw. Kipondya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Mtakatifu Therese, iliyopo Ukonga, amewataka wananchi kuendelea kuchangia shule zilizopo ndani ya kata hiyo ili kuboresha mfumo wa elimu.

Alisema shule hiyo inahitaji sh. bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala hivyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.


No comments:

Post a Comment